0
Msanii Roma Mkatoliki asema anahofia maisha yake siku moja tu baada ya kupatikana katika kituo cha polisi cha Oysterbay.
Akizungumza na vyombo vya habari akiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, msanii huyo ameelezea vile walivyotekwa siku ya Jumatano na kufungwa pingu na kitambaa usoni na baadaye kusafirishwa hadi eneo wasilolijua.
Akizungumza na hisia na uchungu mwingi Roma alisema kuwa walipofikishwa walipopelekwa walipata mateso mengi kwa kupigwa hadi siku ya Ijumaa usiku.
Roma Mkatoliki: Tukatolewa tulimokuwepo siku ya ijumaa jioni na kufungwa uso, na mikono na miguu. Tukapelekwa sehemu tukatupwa kwenye dimbwi la maji karibu na baharini Roma anasema kuwa alipata fahamu na kuweza kuwafungua wenzake na kutembea mwendo mrefu ambapo walifika katika maeneo ya Ununio.
Hatahivyo msanii huyo alishindwa kuelezea baadhi ya maswali aliyoulizwa kuhusu mahojiano na waliowateka huku akisema tu kwamba tayari wamewasilisha malalmishi yao kwa polisi kwa uchunguzi.
Harakati za waandishi za kumtaka azungumze kuhusu mahojiano hayo ziligonga mwamba huku maafisa wa serikali walioandaa mazungumzo hayo na wanahabari wakimzuia msanii huyo kusema lolote .
Awali Roma na wenzake walionyesha baadhi ya majeraha waliyopata chini ya watu waliowateka na kusisitiza kwamba kile walichokipitia sio suala la mzaha.
Wameitaka serikali kuwahakikishia usalama wao wakidai kwamba licha ya kuwepo katika eneo lililozungukwa na watu maarufu ikiwemo serikalini watekaji wao walifanikiwa kutekeleza tendo hilo bila wasiwasi.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top