Chama
cha ACT Wazalendo kimelaani vikali hatua za jeshi la polisi nchini
kutumia nguvu kuwatawanya watu wenye ulemavu ambao walikuwa wameandamana
Ijumaa katika barabara ya Sokoine, Posta Jijini Dar es salaam ili
kwenda kumuona Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala.
Walemavu
hao walikuwa wamefanya maamuzi hayo ili kukutana na Mkurugenzi wa
Manispaa ya Ilala kwa lengo la kuwasilisha malalamiko yao kutokana na
watu hao kukamatwa na kuzuiliwa kuingia mjini.
"Chama
cha ACT Wazalendo kinalaani vikali na kwa nguvu zote kitendo cha jeshi
la polisi kutumia mabomu ya machozi na virungu dhidi ya watu wenye
ulemavu wasio na silaha yoyote. Katika tukio husika lililotokea Juni 16,
2017 jijini Dar es salaam, askari wa jeshi la polisi waliwavamia,
kuwapiga, kuwaswaga na kuwaburuza watu wenye ulemavu kwa kisingizio kuwa
hiyo ilikuwa njia ya kurahisisha kukamatwa na kutawanywa kwao" Alisema Ado Shaibu
Chama
Cha ACT kinasema kuwa wao wanaamini kuwa jeshi la polisi lingeweza
kuwakamata au kuwatawanya walemavu pasipo kutumia nguvu yoyote zile kwa
kuwa watu hao hawakuwa na silaha zozote zile, ACT wanasema kitendo hiki
cha polisi hakivumiliki hata kidogo.
"ACT
Wazalendo tunaamini kwa dhati kabisa kuwa jeshi la polisi lingeweza
kuwakamata na kuwazuia watu hao wenye ulemavu, ambao hawakuwa na silaha
yoyote, bila kutumia nguvu kubwa kama walivyofanya. Pia, badala ya
kuwatawanya na kuwakamata, jeshi la polisi lingeweza kuwaongoza walemavu
hao hadi Manispaa ya Ilala walikotaka kwenda kuwasilisha kilio chao.
Vitendo hivi vya polisi kutumia mabavu na nguvu kubwa hata kwenye
mazingira ambayo njia nyingine zingeweza kutumika havivumiliki hata
kidogo" alisisitiza Ado Shaibu
Mbali
na hilo ACT Wazalendo wamemtaka Waziri mwenye dhamana ya jeshi la
polisi kuomba radhi kwa Jumuiya ya watu wenye ulemavu huku Waziri mwenye
dhamana ya watu wenye ulemavu wakimtaka kuhakikisha kuwa madai ya
walemavu yanafanyiwa kazi.
"ACT
Wazalendo tunamtaka Waziri mwenye dhamana ya jeshi la polisi, Waziri wa
Mambo ya Ndani, ndugu Mwigulu Nchemba kuiomba radhi jumuiya ya watu
wenye ulemavu hapa nchini kwa kitendo cha jeshi la polisi na kuhakikisha
vitendo kama hivi havirudiwi tena. Pia tunamtaka Waziri mwenye dhamana
ya watu wenye ulemavu, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Walemavu Ndugu Jenister Mhagama kuhakikisha madai ya watu hawa wenye
ulemavu yanasikilizwa na kutolewa majawabu" alisisitiza Ado Shaibu
Kwa
kumalizia Ado Shaibu ambaye ni Katibu mwenezi wa ACT Wazalendo Taifa
aliitaka jamii kiujumla kuzingatia misingi yetu ya Utu, Upendo na Udugu,
kusimama pamoja na watu wenye ulemavu kukipinga kitendo hiki cha
kuwavunjia utu wao.
Post a Comment
karibu kwa maoni