SERIKALI imeendelea
kupata neema kutokana na uwekezaji wake kwenye mashirika na taasisi mbalimbali yanayojiendesha
kibiashara nchini ambapo leo Shirika la Bima la Taifa (NIC) limetoa gawiwo la
Shilingi bilioni 1.707 baada ya kupata faida kiabishara mwaka 2016/2017.
Kwa nyakati tofauti
mwaka huu, Serikali ilipokea kiasi cha Shilingi bilioni 1.7 kutoka Benki ya
Taifa ya Biashara (NBC) na kufuatiwa na NMB Bank Plc, iliyotoa kiasi cha
Shilingi bilioni 16.5 hivi karibuni.
Akipokea Hundi
kifani ya kiasi hicho cha Shilingi 1.707 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika la Bima la Taifa, Bw. Sam Kamanga, Waziri wa Fedha na Mipango, amelipongeza
shirika hilo kwa kuonesha maendeleo makubwa katika kipindi kifupi tangu azindue
Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo mwishoni mwa mwaka uliopita.
“Nilipozindua Bodi
yenu ya Wakurugenzi uliniahidi Mkurugenzi Mtendaji kuwa mtafanyakazi kwa bidii
na kuanza kutoa gawiwo Serikalini, ninajisikia furaha sana kwa niaba ya
watanzania kuona kuwa mnatimiza ahadi hiyo kwa kutoa asilimia 15 ya pato ghafi la
mapato yenu. Nawapongezeni sana” alisisitiza Dkt. Mpango.
Alizitaka taasisi
nyingine za umma zilizochini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina zinazofikia 260 kuanza
kutumia huduma za bima kupitia Shirika la Bima la Taifa.
Alisema anafahamu
kwamba kuna taasisi nyingine zina mikataba na mashirika mengine ya bima lakini akatoa
wito kwa taasisi hizo kwamba baada ya kumaliza mikataba yao, waanze kupata
huduma kupitia NIC ambalo manufaa yake yameanza kuonekana baada ya kuanza
kurejesha sehemu ya faida yake kwa Serikali.
Hata hivyo Dkt.
Mpango aliitaka NIC lisibweteke badala yake liboreshe huduma zake ili kuweza
kujiongezea soko kwani mashirika ya bima yamekuwa na ushindani mkubwa.
Alilitaka Shirika
hilo kutoa elimu kwa Umma wakiwemo wakulima, wafugaji na wananchi wengine kuhusu
umuhimu wa kukatia bima mifugo, mazao, nyumba na vyombo vya moto ili kujiepusha
na hasara zinazoweza kutokea wakati wa majanga.
Kwa upande wake Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alisema kuwa tukio
hilo ni la kihistoria kwa Shirika hilo kutoa gawiwo kwa Serikali tangu lianzishwe
miaka 54 iliyopita na kuzitaka Taasisi zote zilizo chini ya Wizara kuiga mfano
wa NIC.
“Naamini leo ndiyo
mmezaliwa na mna miaka mingine 100 mbele ya kutenda kwa ajili ya watanzania”
Alisisitiza Dkt. KIjaji
Naye Katibu Mkuu wa
Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Dotto James alilipongeza Shirika hilo na
kusisitiza kuwa Wizara ipo bega kwa bega kushirikiana nao ili kuhakikisha
Shirika hilo linapiga hatua zaidi kwa maendeleo ya Taifa.
Akizungumza kabla
ya kukabidhi hundi kifani, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima ya Taifa (NIC), Bw. Sam Kamanga, aliishukuru
Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuzihamasisha Taasisi za Umma kukata bima NIC, na
kwamba hatua hiyo ndiyo imeliwezesha shirika kutengeneza faida na kutoa gawiwo
kwa Serikali.
Hata hivyo ameiomba
Serikali kuyahamasisha mashirika zaidi ya 200 yaliyochini ya Msajili wa Hazina
kutumia huduma za Taasisi yake ili kuongeza wigo wa mapato na kuleta faida
zaidi kwa wabia wa Shirika hilo
“Ni Taasisi 15 tu
ndizo zilizoitikia wito wa Serikali wa kutumia huduma za bima kupitia NIC
lakini mashirika na taasisi nyingine bado hivyo ninaiomba Serikali itusaidie
kufanikisha jambo hili” Alisistiza Bw. Kamanga.
Aliiahidi Serikali
kwamba Shirika lake linatarajia kuongeza gawiwo zaidi za kiasi hicho kilichotolewa
kutokana na mikakati kabambe ya kiabiashara waliyojiwekea.
Post a Comment
karibu kwa maoni