WAZIRI
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amefanya ziara ya kushitukiza katika
Kituo cha Forodha Bandarini, kilichoko katika Bandari ya Dar es Salaam na
kuiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, kufanya mabadiliko makubwa ya
watumishi walioko katika idara ya upimaji na ukaguzi wa mizigo baada ya
kubainika kuwa baadhi yao wanajihusisha kwa namna moja au nyingine na upotevu
wa mapato ya Serikali.
Dokta
Mpango ametoa muda wa siku saba kwa TRA kumpa taarifa kamili ya utekelezaji wa
maagizo hayo, ikiwemo kuwahamisha watumishi wote waliokaa muda mrefu kwenye
eneo hilo la upimaji na ukaguzi wa mizigo ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji
mapato ya Serikali katika Bandari hiyo.
Ameshangazwa
na kitendo cha Mapato katika Bandari ya Dar es Salaam kutoongezeka licha ya
juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, kuboresha Bandari hiyo
kutokana na baadhi ya watumishi wasio waaminifu kushirikiana na wafanyabiashara
wasio waaminifu kukwepa kodi ya serikali.
“Pamoja
na kuwepo kwa mitambo ya kukagua mizigo (Scanners), baadhi ya bidhaa
zinakadiriwa kodi ndogo ikilinganishwa na thamani ya mizigo huku mizigo mingine
ikiwa si ile iliyotajwa kuwemo kwenye makontena na hupitishwa na watumishi
wasio waaminifu” alisisitiza Dokta Mpango.
Aidha,
Waziri huyo wa Fedha na Mipango ameuagiza ungozi wa TRA kuhakikisha kuwa wanaongeza
mapato katika bandari ya majahazi kutoka wastani wa mapato ya shilingi bilioni
3.5 kwa mwezi hadi shilingi bilioni 5, kulingana na malengo yaliyowekwa baada
ya kubainika kuwa kuna ukwepaji mkubwa wa mapato ya Serikali katika eneo hilo.
Dokta
Mpango ameuambia uongozi huo wa Mamlaka ya Mapato nchini TRA kuhakikisha kuwa Bandari
ya Majahazi ianze mara moja kutumia mfumo wa kukusanya mapato ujulikanao kama
TANSIS ili kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi.
Post a Comment
karibu kwa maoni