Wakati Rais John Magufuli akitoa ajira mpya 3,000 jeshini, Mkuu wa Majeshi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo amewataka wanajeshi kutojihusisha na matumizi mabaya ya mitandao kwa kuwa ni kinyume na kanuni za ulinzi wa Taifa.
Ajira hizo mpya ni sehemu ya
mkakati wa Serikali wa kuwa na jeshi imara na la kisasa ili
litakalofanya kazi ya ulinzi wa nchi kwa ufanisi.
Akizungumza
baada ya kutunuku kamisheni kwa maofisa 422 wa JWTZ kundi la 61, Rais
Magufuli alisema lengo la nafasi hizo ni kuhakikisha jeshi linakuwa na
askari wa kutosha.
Alisema, “Jeshi haliwezi kuwa na
maofisa tu, tutaongeza na askari wa kawaida, wengi watakaopata nafasi
hizi nataka wawe wamepitia JKT, tunataka tujenge jeshi la kisasa. Kuhusu
changamoto ndogondogo msiwe na wasiwasi tutazishughulikia na wiki ijayo
tutaanza kufanyia kazi madai yenu.”
Rais Magufuli
alisema utawala wake umekuwa na imani kubwa na jeshi ndiyo sababu
amekuwa akiwateua wanajeshi katika nafasi mbalimbali za uongozi ili
walete maendeleo kwa haraka.
“Nilipoingia madarakani na
kuanza kuteua wanajeshi katika nafasi mbalimbali kuna watu walianza
kunishangaa na wapo ambao walisema nataka kuifanya nchi ya kijeshi.
Nawapenda wanajeshi kwa sababu wanapeleka mambo kwa haraka, ndiyo sababu
niliwateua ili mambo yaende kasi na ninaona jinsi wanavyochapa kazi na
kupeleka mambo harakaharaka.”
Mbali ya suala hilo la
ulinzi, Rais Magufuli pia alizungumzia mambo mengine ya kimaendeleo
akiwataka Watanzania kuacha kujihusisha na kilimo cha bangi na badala
yake wajikite kwenye kilimo cha mazao ya chakula na biashara.
Alisema
dawa za kulevya zinawaharibu vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa
hali inayosababisha wengi wao kushindwa kufanya kazi.
“Hatuwezi
kuwa tunatengeneza Taifa la watoka udenda. Hao hata uwape kazi gani
hawataweza kufanya. Ukimpeleka kiwandani mashine zinaweza kumkata
mikono, vijana acheni masuala ya madawa ya kulevya ni lazima tutengeneze
Taifa lenye mwelekeo ili siku moja Tanzania iwe nchi ya kutoa misaada.”
Aliwasisitiza wakazi wa Arusha kuendelea kuchapa kazi na kutokubali kutumiwa na wanasiasa kwani maendeleo hayana chama.
“Msikubali
kuyumbishwa na itikadi za vyama, tushikamane kuleta maendeleo na
kutunza amani yetu. Wengine wanawapa viroba mnaandamana ndiyo sababu
tumeamua kuviondoa, vijana mchape kazi. Mimi naweza kusimama na kusema
Chadema oyee na nikaweka vidole kwa ishara wanayoweka kwani
nitapungukiwa nini! Hizo alama hazina faida kama una njaa,” alisema.
Kuhusu
mwenendo wa uchumi Rais Magufuli alisema Tanzania imeanza kubadilika na
kasi yake ya ukuaji uchumi inaifanya kuwa miongoni mwa nchi tatu za
Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa haraka.
“Wanaolalamika
hela hakuna ni wezi. Sasa hivi mzunguko wa fedha umekaa vizuri, hapo
awali zilikuwa nyingi mtaani kwa sababu zilikuwa za wizi lakini sasa
thamani yake inaonekana, najua tunavyopambana hivi kuna watu hawapendi
wanaumia kwa sababu walikuwa wakila jasho la Watanzania.
“Nimeamua
niwe sadaka ya Watanzania kwa ajili ya kuwanyoosha mafisadi. Hamjui
mateso ninayopitia, ni shida kuwa Rais, nimeyaona mateso kuwa Ikulu,
niliomba kwa kujaribu nikasukumwa huko. Sababu niliingia bila kutoa
rushwa lazima nifanye kazi kwa ajili ya Watanzania hakuna fisadi
aliyenichangia hela hivyo sitaogopa kumtumbua yeyote na nitawatumbua
kwelikweli.”
Kuhusu kwenda nje ya nchi Rais Magufuli
alirejea kauli yake kwamba amepata mialiko mingi kutoka kwa mashirika na
wadau mbalimbali wa maendeleo lakini haendi kwa sababu anafanya kazi ya
kujenga nchi.
“Kila mara wananialika nimeshaacha
mialiko karibu 60. Niende huko kufanya nini? Nasafisha kwanza hapa,
nikienda huko kutaharibika, nasafisha nyumba yangu, niliomba urais wa
Tanzania siyo wa kutembelea nchi za watu. Kama kutembea nilitembea
wakati nasoma nchi zote hizo nilifika sasa nimeamua kuchapa kazi. Fedha
nyingi za Watanzania zilitumika kwenye safari, kuna watu walikuwa
hawatulii wanapishana tu angani.”
Kuhusu Serikali
kuhamia Dodoma, Dk Magufuli alisema anataka ifikapo mwakani watumishi
wote wa umma wawe wamehamia makao makuu ya nchi.
“Nimesema
watu wahamie Dodoma, mimi mwenyewe naenda mwaka kesho... sasa
atakayebaki Dar abaki na kazi hamna. Nashangaa kwa nini hawataki kwenda
Dodoma wakati tumejenga barabara nzuri.”
Jenerali Mabeyo
Awali,
Jenerali Mabeyo aliwataka maofisa hao waliotunukiwa kamisheni kufanya
kazi kwa uzalendo, utii, kuheshimu na kulinda Katiba ya nchi.
“Kutunikiwa
kamisheni ni ishara ya kupewa dhamana ya uongozi, niwasihi sana
kuheshimu, kuthamini na kuzingatia kiapo cha utii mlichoapa leo mbele ya
Amiri Jeshi Mkuu. Mkumbuke kiapo hiki ndicho kinacholinda Sheria ya
Ulinzi wa Taifa ambayo ndiyo imetoa kanuni za ulinzi wa Taifa.
“Bahati
mbaya wapo baadhi ya maofisa na askari wanaosahau haraka na kuanza
kukiuka kiapo chao, naomba urejee matamshi uliyoyatoa leo, yanaelekeza
wajibu wako, utii, kuilinda Katiba pamoja na kumtii Rais.”
Kuhusu
matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, Jenerali Mabeyo alisema
kumekuwapo na baadhi ya wanajeshi wanaojihusisha na vitendo hivyo
vinavyokiuka kanuni na taratibu za JWTZ.
“Wajibu wa
kwanza wa jeshi letu ni kuilinda nchi, wananchi na mali zao, tuwe macho
na matishio yaliyopo katika zama hizi ambayo yanatoka ndani na nje ya
nchi, ni vyema tukayaona hayo na kuwa tayari kukabiliana nayo mahali
popote na wakati wote.
“Endeleeni kuwa na uzalendo,
imarisheni uhusiano mzuri na wananchi, epukeni kwa namna yoyote ile
kuliingiza jeshi kwenye siasa kwani kufanya hivyo ni hatari kwa ustawi
wa Taifa letu,”
Jenerali Mabeyo alisisitiza kuwa nchi
iko salama na kuwataka Watanzania wote kuwa tayari kuilinda nchi yao kwa
kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.
Post a Comment
karibu kwa maoni