Tanzania
imetoa rai kwa Serikali ya Uingereza kubadili mfumo wa uhusiano wake
kwa kujikita zaidi katika masuala ya biashara na uwekezaji badala ya
kutoa misaada ya kawaida ili nchi iweze kukuza uchumi wake kwa haraka
zaidi.
Wito
huo umetolewa Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Isdor Mpango, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa
wabunge kutoka mabunge ya uingereza (Baraza la Mamwinyi na Bunge la
Wawakilishi).
Dokta
Mpango amesema kuwa kiwango cha mtaji ambacho Serikali ya Uingereza
imewekeza nchini hadi sasa ni Paundi bilioni 2.5 lakini kwa upande wa
biashara kati ya nchi hizo mbili, hali si nzuri.
"Mwaka
2015 Tanzania iliuza nje bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani
milioni 22.5 na kununua bidhaa kutoka Uingereza zenye thamani ya Dola
milioni 150, kiwango ambacho ni kidogo sana na tunahitaji kufanya
biashara zaidi" Alisisitiza Dkt. Mpango.
Alielezea
hatua mbalimbali ambazo Serikali inazichukua kuimarisha uchumi wa
viwanda na kuelezea changamoto kubwa ikiwa na namna ya kuendeleza kilimo
kwa ajili ya kupata malighafi za viwanda na kuwainua wananchi kiuchumi
kwa kuwa kilimo ndicho kinaajiri idadi kubwa ya Watanzania.
Dkt.
Mpango alitoa wito kwa Serikali ya Uingereza kuwekeza zaidi katika
viwanda vitakavyoongeza thamani ya bidhaa mbalimbali ikiwemo kujenga
viwanda vya kutengeneza matrekta na zana nyingine za kilimo, kusindika
bidhaa za mazao ya wakulima pamoja na kuwekeza katika sekta za kuongeza
thamani ya madini na nishati ya umeme.
Dokta
Mpango aliwaeleza Wabunge hao kwamba hivi sasa Serikali imepiga hatua
kubwa kiuchumi na kuishukuru Uingereza kwa mchango mkubwa inaoutoa
kusaidia Elimu, Lishe, Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma na afya
kwa upande wa lishe, uwekezaji ambao kwa pamoja umefikia zaidi ya paundi
milioni 180.
Kwa
upande wake, kiongozi wa Wabunge watano waliomtembelea Waziri wa Fedha
na Mipango, Mheshimiwa David Linden, amesema wamefurahishwa na namna
Tanzania inavyopiga hatua kubwa kimaendeleo na kudhibiti vitendo vya
rushwa.
Amesema
kuwa wameridhishwa na kiwango cha miradi wanayoifadhili katika sekta ya
elimu na afya hususan masuala ya lishe kwa watoto na kwamba nchi yao
itaendelea kuisaidia Tanzania ili iweze kufikia malengo yake kiuchumi na
kijamii
Wabunge hao wapo nchini tangu Jumapili iliyopita na wanatembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Serikali ya Uingereza.
Post a Comment
karibu kwa maoni