Siku 10 baada ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi, familia yake imezungumzia tukio hilo na namna inavyomfahamu dereva wake kwa zaidi ya miaka 20.
Tangu
kutokea kwa tukio hilo mchana wa Septemba 7 huko Dodoma, dereva wa
mbunge huyo, Simon Mohamed Bakari amekuwa akitajwa kama mtu muhimu
anayeweza kusimulia tukio hilo na hata kusaidia kuwabaini wahalifu.
Hata
polisi imekuwa ikimtaka ili imhoji ikisema ni shahidi muhimu katika
tukio hilo. Hata hivyo, kijana huyo yupo Nairobi akimuuguza bosi huku
mjadala juu yake ukiendelea nchini.
Katika mahojiano na
Mwananchi, familia ya mbunge huyo imeonyesha kuwa na imani kubwa na
dereva hiyo ikibainisha inavyomfahamu kwa miongo miwili.
Akizungumza
katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwa baba wa mbunge huyo,
Lissu Mughwai katika Kijiji cha Mahambe, Kata ya Unyahati wilayani
Ikungi, Singida, Muro Lissu ambaye ni kaka yake alisema hawana wasiwasi
na dereva huyo kwa kuwa ni kijana aliyelelewa na mwanasheria huyo mkuu
wa Chadema tangu akiwa na umri wa miaka 15.
“Yule
kijana alienda kwa Lissu akiwa mdogo kama kijana wa kazi za nyumbani.
Alimchukua katika Kijiji cha Sefuka kilichopo Magharibi mwa Singida.
Tangu wakati huo alimfunza kazi zote akiwa pale nyumbani kwake. Amemlea,
amekulia kwake,” alisema Muro.
Alisema dereva huyo alifundishwa mambo mengi akiwa mmoja wa wana familia ikiwamo kupelekwa kujifunza udereva.
Muro alisema Lissu alipoanza harakati za kuwania ubunge mwaka 2007 alikuwa na kijana huyo.
“Amekuwa
dereva wake tangu alipoanza kuhangaikia jimbo mpaka amechukua ubunge
mwaka 2010 akawania tena 2015. Wana miaka mingi na yule kijana zaidi ya
miaka 20 amemlea,” alisema Muro.
Alisema licha ya Lissu
kutozungumza chochote kuhusu vitisho alivyokuwa akipewa na kufuatiliwa
na watu wasiojulikana, dereva wake alikuwa akiitaarifu familia kuhusu
matukio hayo kila yalipotokea, hivyo walijua kinachoendelea kupitia
kwake.
Katibu wa Chadema Wilaya ya Ikungi, Jihala
Ibrahim aliyekuwapo pamoja na wanafamilia katika mahojiano hayo alisema
licha ya kuchanganyikiwa, dereva huyoalielezea tukio zima lilivyokuwa
baada ya wao kuwasili hospitalini Dodoma wakitokea Ikungi.
“Nilikutana
na dereva wake Dodoma baada ya tukio, kwa kweli yule kijana alikuwa
amechanganyikiwa na mpaka anaondoka siku ya pili kwenda Nairobi alikuwa
ameathirika kisaikolojia,” alisema.
Ibrahim anaamini
kuwa kama asingekuwa dereva huyo, Lissu asingepona kirahisi, “Dereva
wake anasema tangu wanatoka bungeni, magari mawili yalikuwa
yakiwafuatilia na kila alipojaribu kuegesha gari pembeni na wao
walifanya hivyo hivyo aliamua kwenda moja kwa moja nyumbani na
walipofika getini gari moja lilibaki nje na lingine liliingia ndani.”
Ibrahim
alisema dereva huyo aliwaeleza kuwa kabla ya watu hao kutekeleza azma
yao, Lissu alikuwa tayari kushuka lakini alimzuia licha ya kutaka
kushuka kwa nguvu.
“Dereva alisema baada ya kimya
kifupi, gari hilo liligeuza tayari kwa kuondoka hapo alishuka mmoja wa
watu hao akiwa ameficha uso wake kwa kofia na miwani myeusi, alitoa
silaha na kuanza kushambulia gari la Lissu. Dereva alimwinamisha Lissu
kwa nguvu kupitia nafasi iliyopo kati ya kiti chake na yeye na alifungua
mlango na kujificha chini ya uvungu wa gari nyingine iliyokuwa
pembeni,” alisimulia Ibrahim.
Alisema kutokana na hali ambayo alikuwa nayo kijana huyo, walilazimika kumwondoa hospitalini hapo na kumhifadhi.
“Siku
ya pili baada ya Lissu kupelekwa Nairobi, dereva wake aliletwa sababu
siku ya tukio makamanda wa Chadema Dodoma walimhifadhi na baadaye
tulimpeleka Nairobi kupata matibabu ya kisaikolojia kwa kuwa alikuwa mtu
wa kwanza kushuhudia damu ya Lissu ikimwagika,” alisema.
Kauli kwa familia
Muro
alisema mdogo wake hakuwa mwepesi wa kuzungumza yanayomkabili, lakini
kuna siku alizungumza kauli yenye utata ambayo amekuwa akiifikiria.
Alisema
akikariri maneno ya Lissu, “Kuna wakati nafikiria tupo kwenye tanuru la
moto wa mkaa wa tofali kama unaweza kutokea huku na huku tanuru
linawaka ni kazi ngumu mbele yangu, kama nakanyaga tanuru nitokee upande
wa pili.”
Muro alisema hakumjibu lakini alishangaa ni kwa nini alitoa kauli hiyo.
Alisema japokuwa familia ilikuwa inaona anachokifanya ni kizuri, lakini yeye Muro kuna wakati alikuwa akiwaza.
Muro
alisema wiki mbili kabla ya tukio hilo, Lissu alikutana na familia yake
alipohudhuria mazishi ya kaka yao na kwa kipindi chote walichokaa naye
hakusema lolote.
“Baada ya kukutana, tumekaa, tumezika
mpaka tukafanya kikao jioni cha ukoo kwa kweli hakuzungumza lolote na
tangu alipotoka huku hatujawasiliana naye,” alisema.
Shambulio la risasi
Muro
alisema tukio la Lissu kushambuliwa lilimshtua kila mwanafamilia na
mpaka sasa hawajui cha kufanya na zaidi ya kusubiri taarifa kutoka kwa
vyombo vya ulinzi na usalama.
“Mimi nafanya kazi pale
Ikungi, siku hiyo nilikuwa nimepumzika saa saba hivi watoto wakaja mbio
wakaniambia baba; baba mdogo kapigwa risasi niliruka sababu nilikuwa
usingizini, sentensi ya kwanza ilikuwa amekufa? Walinijibu subiri
kidogo,” alisema.
Muro alisema alipoambiwa kuwa amepelekwa hospitali Dodoma alipumzika kwa nusu saa baadaye akaamua kuelekea huko.
“Nilipofika
Manyoni nilipigiwa simu kuambiwa nirudi maana hata ningefika
nisingeweza kumuona kwa kuwa wanafanya utaratibu wa kwenda Nairobi,
Nilirudia hapo. Familia tumepigwa na mshangao na mpaka sasa japokuwa
tunasikia kwamba hali yake ni nafuu lakini tumelipokea suala hili kwa
mshtuko mkubwa ,” alisema.
Alisema baba yake mdogo,
shangazi zake, mama zake wadogo, binamu zake na hata wapigakura wake wa
Ikungi na wananchi kwa jumla walipigwa na bumbuazi.
Muro
alisema familia imewatuma ndugu akiwamo kaka yake Alute ambaye ni
mwanasheria jijini Arusha, mjomba wao na dada yao anayeishi Songea
kwenda Nairobi kufuatilia hali yake.
“Kule kuna dereva
wake ambaye yupo karibu na sisi, mke wake na watu wengine ambao ni
viongozi wa chama wapo kule. Kuna dada yetu anayekaa Songea na kesho
anaondoka mdogo wetu anaitwa Vincent, ni muda mfupi hatujafikiria
tufanye nini,” alisema.
Muro alisema mwishoni mwa mwezi huu watafanya kikao Dar es Salaam wajue nini cha kufanya.
Baba
mdogo wa Lissu, Muro Sawa (79), alisema kitu ambacho wazazi
wangefurahia ni kumwona kijana wao akirudi nyumbani akiwa mzima.
“Familia
tutakaa kikao kushauriana ili tujue suala hili tunalitatua vipi, lakini
niiombe Serikali kumzidishia ulinzi kijana wangu. Sisi familia tuna
uchungu mkubwa kuhusu hili,” alisema Sawa.
Shangazi wa
Lissu, Ninaa Sawa Muro (83) alisema, “Tunakula chakula hakishuki,
matonge yanakaba shingoni, maungo yote yanauma kwa sababu ya mtoto wetu,
tangu siku ile niliposikia nilikuwa kwenye kiti ghafla nikaanguka na
kuanza kutetemeka.”
Alisema alijisikia vibaya baada ya
kuambiwa na mtoto wake taarifa hizo, “Aliniuliza umesikia kwamba Tundu
Lissu amepigwa risasi? Nikanyamaza, nikaona joto. Kwa jinsi shangazi
yangu anavyonipenda hata anikute Manyoni hata Dar es Salaam ananiita
jina langu la kikwetu anakuja ananikumbatia iliniuma sana.”
“Alifanywa
hivyo kwa nini? Kama tunavyojiona wote roho moja tumfikirie huyo Tundu
Lissu,” alisema shangazi huyo ambaye baada ya baba yake Lissu kuzaliwa
ndiye aliyemfuata.
Mama mdogo wa Lissu, Bula Muro, alisema baada ya kupata taarifa alianguka chini na kuanza kulia hakufikiria kama amepona.
Mitandao ilivyoiliza familia
Mmoja
wa wanafamilia, Msengi Ntandu Mughwai alisema walipata shida siku hiyo
ya tukio, “Tulipanga kwenda Dodoma wakasema turudi anaendelea na
matibabu, tulihisi wanatudanganya sababu mtandaoni wanasema hali mbaya
na kwa kuwa walikuwa ni wanafamilia waliotushauri, tuliamua kurudi usiku
kwa kweli kesho yake kulikuwa na habari za ajabu kwenye mitandao yaani
zilituumiza sana,” alisema.
Msengi alisema walikuwa
wakipigiwa simu na kupewa taarifa zenye utata na wakiingia mitandaoni
wanaona habari za ajabuajabu na kwamba hali kwao ilikuwa mbaya.
“Kwa
kweli tulipata shida, wazazi wetu walikuwa wanakuja mara kwa mara
tunawajibu kwamba anaendelea vizuri lakini wazee wetu walikuwa wanapata
taarifa mbaya kwingine kutokana na mitandao ya kijamii,” alisema.
CHANZO:MWANANCHI
CHANZO:MWANANCHI
Post a Comment
karibu kwa maoni