Ni jambo la nadra kwa wananchi kuwagomea viongozi wa juu wa Serikali, hususan wanapokutana nao ana kwa ana, lakini Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amegomewa na kulazimika kuunda kamati kuchunguza madai yao.
Mara nyingi,
wananchi wanapokuwa na madai yao huomba yatatuliwe, lakini ni nadra
kuwakatalia viongozi wakisisitiza kupatiwa haki wanazotaka.
Hata
hivyo, wananchi wa Kitongoji cha Saitabau kilichopo katika Kata ya
Tarakwa wilayani Arumeru wamegoma kujiunga na Mamlaka ya Mji mdogo wa
Ngaramtoni na kuruhusu mradi wa maji katika kijiji chao kuwa chini ya
mamlaka hiyo.
Kutokana na mgomo huo, Gambo ameamua kuunda kamati ya wataalam kutoka ofisini kwake ili kuchunguza mgogoro huo.
Wakizungumza
na Gambo aliyefika katika kitongoji hicho, wananchi hao walisema
hawataki kujiunga na mamlaka hiyo kwa kuwa hawajui faida zake, badala
yake wanachoona ni kunyang’anywa mradi wa maji.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Lucas Lukumai alisema wananchi wanapinga kujiunga na mamlaka hiyo kutokana na kutopatiwa elimu.
Pia,
alisema wanapinga kuhamishwa kwa madai kwamba mamlaka hiyo inataka
kuchukua mradi wao wa maji ambao waliuchangia na kusaidiwa na shirika la
misaada la kimataifa la Oxfam.
“Mimi nilikamatwa na
kuwekwa rumande na polisi kwa agizo la mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri kwa tuhuma za kuikataa mamlaka jambo ambalo si kweli.
Wanaokataa ni wananchi wenyewe kwani hawajapewa elimu,” alisema.
Mwenyekiti
huyo alisema viongozi wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Ngaramtoni walipewa
fursa ya kukutana na wananchi hao ili kuwapa elimu, lakini wameshindwa
kufanya hivyo na badala yake wanawatuhumu viongozi kuwa nyuma ya mgomo
wa wale wanaowaongoza.
Akijibu tuhuma hizo, Mtendaji
Mkuu wa mamlaka ya mji huo, Sophia Shoko alisema wananchi wanagoma
kujiunga na mamlaka kwa kuwa hawataki mradi wao wa maji uwe chini ya
Ngaramtoni.
“Hapa kuna mradi wa maji, wenyewe hawataki
uwe chini ya mamlaka ili maji yasambazwe maeneo mengine na wanataka
kuendelea na malipo ya Sh500 kwa mwezi jambo ambalo si sahihi,” alisema.
Hata
hivyo, Diwani wa kata hiyo, Elihuruma Laizer alimuomba mkuu wa mkoa
kuunda kamati maalumu ya kuchunguza suala hilo na kutafuta nafasi ya
kukaa na wananchi kuwasikiliza kwa kuwa jambo hilo lina mgogoro
alioutaja kuwa ni mkubwa.
Akizungumza baada ya
majadiliano hayo, Gambo alikubaliana na ushauri wa diwani wa kata hiyo
kuunda kamati maalumu ya kuchunguza mgogoro huo kabla ya kuchukua hatua
stahiki.
“Nitaunda kamati ya wataalamu kutoka ofisini
kwangu, watakuja hapa na kuzungumza na wananchi, viongozi wa mamlaka ya
mji mdogo na viongozi wa kitongoji na baadaye watanipa ushauri kufikia
uamuzi,” alisema.
Mamlaka ya Mji mdogo wa Ngaramtoni
iliundwa mwaka 2016 na Halmashauri ya Wilaya ya Arusha ili kupeleka
huduma za kiserikali karibu zaidi na wananchi, lakini ilikutana na
kigingi hicho cha wananchi wanaotaka waachwe waendelee kuwa nje ya
utawala wake.
Post a Comment
karibu kwa maoni