Watu wawili wanaosadikiwa kuwa ni wanachama wa Chadema wanashikiliwa na Polisi Mkoa wa Kinondoni kwa kuhojiwa kuhusu mpango wa maombezi uliopangwa kufanyika katika uwanja wa Tip -Sinza, wilayani Ubungo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Murilo Jumanne aliyekuwa uwanjani hapo na
kikosi cha askari zaidi ya 25 amesema watu hao walikamatwa saa 3:40
asubuhi wakiwa eneo hilo.
"Tunawashikilia na
tutawahoji kama wana uhusiano na kile kilichopangwa kufanyika hapa kwa
sababu kilishapigwa marufuku. Kama hawana uhusiano tutawaachia," amesema
Kamanda Jumanne.
Amesema, “Atakayetaka kujaribu aje
ila cha moto atakiona kwa sababu jitihada za kuzuia watu wema
wasikanyage hapa zimeshafanyika sasa wanakuja kufuata nini."
Katika eneo hilo, polisi walikuwa wakiziondoa bajaji wakiwataka madereva wasiziegeshe hapo kwa siku ya leo.
Baadhi
ya polisi wameonekana wakiwa na mabomu ya kutoa machozi na walifika
uwanjani hapo wakiwa kwenye magari aina ya Toyota Land Cruiser.
Uwanjani hapo hivi sasa ni kweupe kukiwa hakuna maandalizi yoyote kuonyesha kuwa patakuwa na maombezi.
Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo –Chadema
(Bavicha) jana Jumamosi lilitoa taarifa likisema leo litaungana na
viongozi wa kiroho kufanya maombi maalumu kumwombea Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu anayeendelea na matibabu Nairobi, Kenya baada ya
kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7.
Viongozi
wa Bavicha waliofika uwanjani hapo muda si mrefu wamekimbia baada ya
polisi kuwafuata walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari.
CHANZO:MWANANCHI
CHANZO:MWANANCHI
Post a Comment
karibu kwa maoni