Serikali haijazuia matumizi
ya fedha za kigeni nchini bali imechukua hatua ya kudhibiti matumizi ya fedha hizo
ili kulinda thamani ya Shilingi ya Tanzania.
Hayo yalielezwa na Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (MB) alipokutana na wawakilishi
wa wafanyabiashara mkoani Arusha kujadiliana mambo mbalimbali kwa ajili ya kukuza
sekta ya biashara nchini.
Amesema kuwa sheria
haijazuia matumizi ya fedha za kigeni nchini lakini inasisitiza kuwa watu wanapaswa
kutambua kuwa sarafu ndiyo fedha halali kwa malipo ndani ya nchi.
“Tatizo kubwa tunalokumbana
nalo ni uhuru ulioachiwa ambao unasababisha kushuka kwa thamani ya Shilingi yetu
kwani kila mmoja anaweza kutumia fedha za kigeni pia watumiaji wa fedha za kigeni
hawafuati thamani ya fedha iliyoko sokoni kila mmoja anakuwa na kiwango tofauti
cha thamani ya kubadili fedha za kigeni”. alifafanua Dkt. Kijaji.
Ili kuondoa changamoto
hizo Serikali imeamua kurekebisha sheria ya matumizi ya fedha za kigeni na sheria
ya Benki Kuu huku ambayo inazitaka bei zote
hapa nchini zitangazwe kwa Shilingi ya Tanzania. Bei hizi zinajumuisha kodi za nyumba
za kuishi na ofisi, bei za ardhi, gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri
na vifaa vya kielektroniki.
“Bei ambazo walengwa
wake wakuu ni watalii au wateja ambao sio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za
kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni. Hata hivyo kama mlengwa
akitaka kulipa kwa Shilingi ya Tanzania asilazimishwe kulipa kwa fedha za kigeni”
alieleza Dkt. Kijaji.
Aidha, viwango vya kubadilishia
fedha vitakavyotumika katika kuweka hizo bei katika sarafu nyingine vimetakiwa
kuwekwa wazi na visizidi vile vya sokoni.
Mkazi yeyote wa
Tanzania au mtu wa nje anayeishi Tanzania
asilazimishwe kufanya malipo yoyote kwa kutumia fedha za kigeni kama ana
Shilingi ya Tanzania mkononi mfano gharama za shule na hoteli.
Aidha Serikali imeagiza
vyombo vya dola kuchukua hatua za kisheria kwa wote watakaokiuka maagizo hayo yaliyotolewa
na Serikali.
Naibu Waziri Dkt.
Kijaji alitoa rai kwa wafanyabiashara nchini kuhimiza matumizi ya sarafu ili kuweza
kukuza thamani ya Shilingi hivyo kusaidia kuinua uchumi wa nchi.
Post a Comment
karibu kwa maoni