0
MWANAFUNZI wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) aliyepigwa risasi na kufa katika eneo la Kinondoni jijini Dar es Salaam Februari 16, mwaka huu, Akwilina Maftah (22) anaagwa leo jijini Dar es Salaam na atasafirishwa kwenda kuzikwa Moshi.


Serikali na familia ya marehemu wameafikiana kuhusu gharama za mazishi ya msichana huyo.
Jana Serikali ilisema imefikia makubaliano na familia ya Akwilina, kugharamia mambo yote ya mazishi yanayotajwa kisheria na kwamba sasa mipango ya mazishi, inakwenda vizuri.

Makubaliano baina ya serikali na familia ya Akwilina, yalitokana na familia ya mwanafunzi huyo kuwasilisha serikalini bajeti ya mazishi ya Sh milioni 80.

Wanafunzi wa NIT, ndugu, jamaa na marafiki, leo watajumuika kwa pamoja kuanzia saa 7 mchana kumuaga mwanafunzi huyo na baadaye itaanza safari ya kwenda nyumbani kwao Rombo mkoani Kilimanjaro kwa mazishi yatakayofanyika kesho.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, jana ilisema gharama nyingine hazijakubaliwa, kwa vile hazitajwi kisheria. Serikali ilisema pia katika mapendekezo ya familia, yapo pia mambo ambayo yalipewa makadirio ya juu kuliko uhalisia wake.

“Kufuatia hali hii Katibu Mkuu (Dk Leonard Akwilapo) aliagiza kuwe na kikao kati ya Wizara na ndugu wa marehemu ili kuweka sawa changamoto ili kuwe na bajeti ya pamoja, kikao kilifanyika jana jioni (juzi) na kufikiwa muafaka taratibu nyingine za maandalizi ya mazishi zinaendelea,” ilinukuliwa sehemu ya taarifa hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Dk Akwilapo alisema gharama zilionekana kuwa juu na hivyo kuifanya serikali kukutana na Chama cha Kuzikana cha Wazee wa Rombo kilichopo Dar es Salaam kwa majadiliano ya kina.

“Kama ilivyo kawaida ya taratibu za mazishi mahali popote, chama hicho kilikubali serikali kuchangia mahitaji muhimu na si kutoa pesa taslimu.

"Tunaamini kwamba ile bajeti iliandaliwa na vijana, hivyo tukalazimika kuwatafuta wazee ambao tumeelewana vizuri kabisa. Tunaendelea kutoa huduma tangu siku ya Jumapili iliyopita mpaka siku ya mazishi," alisema Katibu Mkuu.

Juzi familia ya marehemu Akwilina ilikabidhi makisio ya bajeti ya zaidi ya Sh milioni 80 kwa ajili ya mazishi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Dk Akwilapo kwa ajili ya utekelezaji, kama ambavyo serikali iliahidi kugharamia msiba huo.

Taarifa hiyo ya familia ilisema watu wanaotarajiwa kusafiri na mwili kwenda kwenye mazishi Rombo ni 300, ambao ni ndugu, jamaa na wanachuo waliokuwa wakisoma na Akwilina.
Bajeti hiyo ilihusisha jeneza Sh milioni 1.5, malipo hospitali Sh 200,000, gari ya kusafirisha mwili Sh milioni 3, magari ya kusafirisha wafiwa makubwa matano Sh milioni 20, chakula njiani Sh milioni 3, chakula kwenye msiba Mbezi kwa siku tatu Sh milioni 10, viti 200 Sh 400,000.

Pia gharama za turubai kwa siku tatu Sh 600,000, Muongoza shughuli (MC) Sh 400,000, picha Sh milioni 1 na maji ya kutumia nyumbani Sh 50,000.

Kwa upande wa Rombo, chakula kwa siku tano Sh milioni 30, muziki na Muongoza shughuli Sh 200,000, turubai Sh milioni 1, viti Sh 400,000, kinywaji cha mabora Sh 100,000, kaburi la kisasa Sh milioni 3, maua na mataji Sh milioni 1, mapambo Sh 500,000 na dharura na tahadhari Sh milioni 2.

Akwilina alifikwa na umauti akiwa kwenye basi, linalofanya safari zake kati ya Mabibo na Makumbusho, lenye namba za usajili T 558CSX Nissan Civilian, ambapo alipigwa risasi wakati gari hilo likiwa eneo la Mkwajuni, Kinondoni wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliokuwa wakiandamana.

Msemaji wa familia hiyo, Festo Kavishe aamesema kuwa familia imepewa na serikali vitu vyote, ambavyo ni vya msingi walivyohitaji kwa ajili ya shughuli za mazishi na kwamba hawana malalamiko yoyote. “Bajeti sijui gharama siyo vitu vya msingi kwa sasa, tunasema familia imeridhika.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top