0
vibuyu-vya-uganga-1IMANI sugu za ushirikiana mkoani Iringa ni mojawapo ya chanzo cha imani potofu zinazochochea vitendo viovu vya ubakaji, ulawiti na udhalilishaji wa watoto wanaoishi katika baadhi ya wilaya za mkoa huo, ikiwemo Iringa Mjini.
Imebainika katika uchunguzi huo kwamba waganga hao hutumia ushawishi wao kuwashawishi watu wazima kubaka na kulawiti watoto kwa lengo la kujipatia utajiri na vyeo.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa hali hiyo imekuwa ikisababishwa na tamaa za kupata mali, fedha na mafanikio kibiashara pamoja na kupandishwa vyeo kazini.
Miongoni wa waganga wa kienyeji aliyeweka bango lake likimnadi kuwa yeye anasafisha nyota na utajiri pamoja na mapenzi mtaa wa Kihesa mjini Iringa na kuambatanisha namba yake ya simu alimshauri mwandishi wa habari hizi kufanya vitendo vya ubakaji kwa watoto wa kike ili kufanikisha malengo yake.
Mganga huyo ambaye namba ya simu imehifadhiwa amenukuliwa akimshauri mwandishi wa habari hizi kumbaka msichana wa umri mdogo ili kusafisha nuksi na pia kufungua njia ya mafanikio.
“Biashara yako ina mkono wa mtu na kwamba unahitaji kujisafisha kutokana na nuksi” aliieleza Mganga kupitia simu yake ya mkononi.
Baada ya Mwandishi wa habari hizi kumtumia kiasi cha fedha Sh 7,700, mganga huyo alimshauri mwandishi kusafisha nyota yake kwa njia ya ubakaji wa binti wa umri mdogo kisha kumlipa kiasi cha Sh 500,000 kwa ajili ya dawa maalum itakayofungua milango ya biashara.
Ofisi ya Ustawi wa Jamii Manispaa ya Iringa Mjini imeeleza kuwa shughuli za waganga wa kienyeji huendeshwa kwa njia za udanganyifu.
Ofisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Iringa Bw. Martini Sitta amesemwa kwamba vipeperushi vya waganga wa kienyeji vimesambazwa katika maeneo mengi Iringa mjini kuvuta wananchi.
Diwani wa Kata ya Mdabulo Ernei Nyeho akiwahutubia wananchi kwenye Mkutano wa hadhara aliwaonya kuhusu waganga wa kienyeji huku akikemea vikali watu wanaochochea vitendo vya ubakaji na ulawiti kuwa ndio njia ya kuelekea mafanikio.
“Waganga hao wanawadanganya kwa vile wanajua wakitoa masharti ya kubaka hutafanikiwa na kwamba utafungwa jela miaka 30 hivyo huwezi kudai fedha ulizowapa” alisema Nyeho.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa David Ngunyale ameeleza kuwa ni vigumu kuingiza ushirikina kama ushahidi unaostahili kutolewa mahakamani.
Hakimu Ngunyale amesema kwamba vitendo vya ushirikina haviwezi kutolewa Mahakamani kama kielelezo cha kuchochea uhalifu wa ubakaji na ulawiti.
Amesema kuwa kesi za ukatili dhidi ya watoto hukwamishwa na wanafamilia kushindwa au kukataa kufungua jalada la mashtaka mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Badala ya kutoa taarifa vituo vya Polisi ili watuhumiwa wakamatwe na kufunguliwa shauri la jinai mahakamani, familia iliyoathirika na uovu huo hukaa chini na kufanya upatanishi kati yake na mtuhumiwa, amesema Hakimu Ngunyale.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top