Mheshimiwa
Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ameondoka nchini jana kwenda London, Uingereza kushiriki kwenye Mkutano
wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) unaotarajiwa kufanyika
kuanzia tarehe 16 hadi 20 Aprili, mwaka huu akimwakilisha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli.
Mkutano
huo ambao Kaulimbiu yake ni “Kuelekea Mustakabali wa Pamoja” utafanyika
chini ya Uenyekiti wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Mheshimiwa Theresa May
na utafunguliwa na Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Malkia Elizabeth wa Pili
wa Uingereza.
Majadiliano
ya Mkutano wa CHOGM 2018 yatajikita kwenye maeneo manne makuu ya
kipaumbele ambayo yatajadili namna Jumuiya ya Madola inaweza kufikia
mustakabali wenye ustawi zaidi; mustakabali endelevu zaidi; mustakabali
wenye haki zaidi; na mustakabali wenye usawa zaidi.
Mijadala
katika maeneo hayo ya kipaumbele itahusisha masuala mbalimbali ikiwemo,
kukuza zaidi biashara na uwekezaji baina ya nchi za Jumuiya ya Madola
kwa manufaa ya nchi wanachama na Jumuiya nzima; kukuza na kuendeleza
misingi ya demokrasia; ajenda ya mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo
endelevu pamoja na masuala ya uhalifu wa kimataifa kama vile ugaidi,
uhalifu wa kimtandao na usafirishaji wa binadamu.
Jumuiya
ya Madola ilianzishwa mwaka 1949 kupitia Tamko la London ambalo
lilikuwa ni matokeo ya Mkutano wa Mawaziri Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya
Madola. Jumuiya ya Madola ina wanachama 53 ambapo kati ya hizo, nchi 19
ni za Afrika, 7 ni kutoka Asia, 13 ni kutoka nchi za Carribean na
Mabara ya Amerika, 11 ni kutoka eneo la Pacific na nchi 3 ni kutoka
Ulaya.
Ujumbe
wa Makamu wa Rais unajumuisha Mheshimiwa Dkt. Balozi Augustine Mahiga
(Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja
na viongozi wengine waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirkiano wa Afrika Mashariki.
Makamu wa Rais na ujumbe wake wanatarajia kurejea nchini Aprili 22, mwaka huu.
Imetolewa na:
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
15/4/2018
Post a Comment
karibu kwa maoni