0
YANGA SC imejiimarisha kidogo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Kwa ushindi huo uliotokana na mabao ya Mzambia Obrey Chirwa na mzawa Simon Msuva, Yanga inafikisha pointi 18 baada ya kucheza mechi tisa ingawa inaendelea kukamata nafasi ya tatu, nyuma ya Stand United na Simba.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na Andrew Shamba wa Pwani, Yanga ilimaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza ikiwa inaongoza kwa bao 1-0, lililofungwa na mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa aliyemalizia kwa kichwa krosi ya Simon Msuva dakika ya 29.
Kwa ujumla, Yanga ilicheza vizuri kipindi cha kwanza ikitawala zaidi sehemu ya kiungo ambako leo ilikuwa inawatumia nyota wake Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite.  
Ubora wa safu ya kiungo Yanga leo uliwafanya hata viungo wa pembeni, Simon Msuva na Deus Kaseke wafanye vizuri pia, kwani walikuwa wanapelekewa mipira kwa wingi.
Washambuliaji wa Yanga, Mzimbabwe Donald Ngoma na Chirwa wangeweza kuifanya timu hiyo ipate mabao zaidi kama wangekuwa makini katika kutumia nafasi.
Safu ya ulinzi ya Yanga nayo ilipewa misukosuko kidogo na washambuliaji chipukizi wa Toto, Waziri Junior na Reliant Lusajo.
Kipindi cha pili, Yanga walirejea vizuri tena na kuendelea kuutawala mchezo.  Haikushangaza winga Simon Msuva alipofunga bao la pili kwa penalti baada ya Kaseke kuangushwa kwenye boksi.
Toto walipata nafasi mbili nzuri zaidi, moja dakika ya 64 wakati Jamal Soud alipowatoka vizuri mabeki wa Yanga, Kevin Yondan na Andrew Vincent ‘Dante’, lakini kipa Deo Munishi ‘Dida’ akwahi kutokea kudaka na nyingine dakika ya 88 wachezaji wa timu hiyo walipomlalamikia kipa wa wapinzani wao kudakia ndani ya mstari mpira mrefu wa Yussuf Mlipili.
Dakika ya 88 Chirwa aliunganishia juu ya lango umbali wa mita mbili baada ta mpira uliotemwa na kipa wa Toto kufuatia shuti la mbali la Kessy.
Kikosi cha Toto Africans kilikuwa; David Kissu, Yussuf Amos, Salum Chukwu, Carlos Protas, Yussuf Mlipili, Ramadhani Malima, Jamal Soud, Reliant Lusajo, Waziri Junior, William Kimanzi na Jaffar Mohammed/Mohammed Soud dk78.  
Yanga leo ni; Deo Munishi 'Dida', Hassan Kessy, Oscar Joshua, Andrew Vincent 'Dante', Kevin Yondan, Mbuyu Twite, Simon Msuva/Matheo Anthony dk86, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma/Thabani Kamusoko dk80, Obrey Chirwa na Deus Kaseke/Juma Mahadhi dk76. 

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top