0
BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM.

Kuzaliwa kwa Nabii Muhammad kuliandamana na miujiza mingi ikiwemo ya kusambaratika kwa nguzo za dhulma na kuzimika moto wa Fars. Nabii Muhammad ambaye jina lake lina maana ya aliyesifiwa, ni mtume wa mwisho kati ya mitume wote waliotumwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kumuongoza mwanadamu katika njia nyoofu kuelekea ufanisi na saada ya milele.

Tunawapongeza wapenda haki na Waislamu wote duniani dunia kwa mnasaba huu adhimu wa kuzaliwa Mtume Mhammad (SAW) pamoja na mjukuu wake Imam Swadiq (AS). Kuzaliwa kwa Nabii Muhammad kuliandamana na miujiza mingi ikiwemo ya kusambaratika kwa nguzo za dhulma na kuzimika moto wa Fars. Nabii Muhammad ambaye jina lake lina maana ya aliyesifiwa, ni mtume wa mwisho kati ya mitume wote waliotumwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kumuongoza mwanadamu katika njia nyoofu kuelekea ufanisi na saada ya milele.

Huyu ni Mtume ambaye alikuwa na siri zote za kuumbwa dunia kwenye kifua chake na kuziongoza nyoyo zilizojaa chuki kwenye njia ya haki na ukweli. Mwenyezi Mungu anasema hivi kuhusiana na Mtukufu huyo: "Amekufikieni Mtume aliye jinsi moja na nyiye, yanamhuzunisha yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni. (Na) kwa walioamini ni mpole na mrehemevu (kabisa) (Tauba 9-128)." Pia amesema: "(Alikuwa) mwenye kuzishukuru neema Zake (Mwenyezi Mungu zilizo juu yake), aka chagua na kumwongoza kwenye njia iliyonyooka (16-121)."

Baada ya Mwenyezi Mungu kumuarifisha Mtume kuwa kiumbe bora zaidi anasema: "Na anachokupeni Mtume basi pokeeni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho (59-7)…." Fadhila na usafi wa ndani ni sehemu ya sifa maalumu za mitume wa Mwenyezi Mungu. Hilo ndilo jambo linalowaunganisha na kuwakurubisha kwa Muumba wao, Mwenyezi Mungu. Watu wema na mashuhuri ambao walibeba bendera ya utume katika historia walifahamika kutokana na ukweli, uaminifu, utakasifu na ulindaji wao wa amana. Wito na ujumbe wao ilifungamana moja kwa moja na wahyi wa Mwenyezi Mungu. Kwa msingi huo, ujumbe wao ulijaa ukweli, mvuto na wala hakuna kasoro au upotovu wowote ulioonekana katika ujumbe wa watukufu hao waliotumwa na Mwenyezi Mungu kuja kuwaongoza wanadamu kwenye njia nyoofu.

Mwenyezi Mungu anaashiria nukta hiyo muhimu na kumtetea Mtume Wake katika aya ya 1hadi 4 za Suratu Najm kwa kusema: "Maapa kwa nyota zinapoanguka, (zinapokuchwa). Kwamba mtu wenu (huyu Nabii Muhammad) hakupotea kwa ujinga wala hakukosa, na hali ya kuwa anajua; Wala hasemi kwa matamanio (ya nafsi yake). Hayakuwa haya (anayosema) ila ni ufunuo, (Wahyi) uliofunuliwa kwake."

Mtume Muhammad alikuwa na maadili na akhlaqi ya hali ya juu kabisa, ambayo haikuwa na mfano wake duniani. Mwenyezi Mungu anaashiria akhlaqi hiyo ya kipekee ya Mtume katika aya ya nne ya Suratu Qalam kwa kusema: "Na bila shaka una tabia njema kabisa." Mtume Muhammad mwenyewe amesema kuhusiana na suala hilo kwamba hakutumwa humu duniani ila kwa ajili ya kukamilisha tabia njema. Kwa msingi huo alikuwa akisisitiza sana juu ya maadili na tabia njema katika mafundisho yake yote kwa wanadamu. Alikuwa akisema: "Mwenyezi Mungu ni Mkarimu, anapenda ukarimu na thamani za kiakhlaki. Huchukizwa mno na vitendo duni na viovu." Pia anasema katika sehemu nyingine: "Jambo zito zaidi katika mizani ya muumini siku ya Kiama itakuwa ni tabia yake njema."

Siku moja kama kawaida, Mtume alikuwa akitembea katika moja ya mitaa na kuuliza: "Nilikuwa na rafiki mmoja ambaye alikuwa akinitupia jivu kila mara nilipokuwa nikipita karibu na nyumba yake. Siku kadhaa zimepita sasa hali ya kuwa simuoni. Kwani yuko wapi?" Watu walimjibu kwa kusema, "yu mgonjwa." Baada ya kusikia hayo, Mtume aliamua kwenda kumtembelea akiwa na masahaba wake kadhaa. Mtu huyo aliaibika sana alipomuona Mtume akimkaribia. Alimwambia mama yake: "Nifunike uso." Mtume alipoingia chumbani kwake, Yahudi huyo alimwambia, "kwanza nisilimishe ili macho yangu yapate kuona kwa kukuona wewe." Yahudi huyo alishangazwa sana na tabia hiyo nzuri ya Mtume, tabia iliyombadilisha kabisa na kumfanya aamue kusilimu." Mtume hata alikuwa akiheshimu na kuwajali watu dhaifu zaidi katika jamii.


Kulikuwa na mwanamke mmoja mweusi ambaye alikuwa akifanya kazi za msikitini mjini Madina. Siku kadhaa zilipita bila ya kuonekana katika sehemu yake ya kawaida ya kazi, jambo lililompelekea Mtume kumuulizia na kumjulia hali. Aliambiwa kuwa alikuwa ameaga dunia. Mtume alihuzunishwa sana na habari hiyo na kuwaambia wafuasi wake kuwa walikuwa wamemuudhi kwa kutompa habari hiyo mapema. Aliamuru aonyeshwe kaburi lake ambapo alienda huko kwa ajili ya kumuombea dua. Alisema kuwa makaburi yana kiza na kwamba hupata mwanga kutokana na dua za waumini.

Katika kipindi chote cha maisha yake, Mtume alikuwa akimtegemea Mwenyezi Mungu tu. Katika vipindi tofauti vya maisha yake na kutokana na busara na uongozi wake shupavu, Mtume nyakati zote alikuwa akipiga magoti, kutukuza, kusifu na kumuomba msaada Mwenyezi Mungu, msaada ambao hatimaye alikuwa akiupata kutoka kwa Muumba wake. Mtume Mtukufu alikuwa mfano bora wa kuigwa na watu katika ukakamavu na ushujaa katika kupambana na batili.

Katika zama za Mtume, kulikuwepo na watu fasidi waliojiona kuwa bora kuliko wanadamu wenzao, ambao walipinga na kukejeli wito wa Mtume wa kuwaita kwenye wongofu, tauhidi, haki na njia ya saada. Licha ya hayo, lakini Mtume hakukata tamaa wala kusitisha juhudi zake za kuwaita watu kwenye wongofu. Aliendelea kusema neno la haki na ksimama imara katika kulitetea.

Lakini mjumbe huyo mwenye huruma wa Mwenyezi Mungu alipoona kwamba Mayahudi wa Bani Nadhir na Bani Qainuqaa ni maadui hatari ambao hawakutaka kuachana na njama na jinai zao dhidi ya Uislamu, aliwafukuza kutoka mjini Madina na kuvunja ngome imara ya Kheibar. Akiwa kwenye ibada tukufu ya hija, Mtume alipiga nara kali ya kujibari na kujiweka mbali na madhalimu na makundi ya batili ili kuwafanya wanadamu katika zama zote wajiweke mbali na madhihirisho ya ufisadi na upotovu. Kwa kufanya juhudi na bidii kubwa, Mtume Mtukufu (SAW) hatimaye alifanikiwa kukabiliana vilivyo na vikwazo muhimu njiani na hivyo kuweza kuwaongoza wanadamu kwenye haki na hakika.


Iwapo tunataka kuwa na sera madhubuti na iliyo wazi kuhusiana na suala la serikali na siasa tunapasa kuiga siasa za serikali ya Mtume Mtukufu (SAW). Hii leo ulimwengu umejiweka mbali sana na misingi ya maadili, umaanawi na uadilifu. Kwa hivyo tunawajibika kuiga busara na sera alizotumia Mtume (SAW) katika kuendesha jamii, ili kufanikisha uendeshaji wa mambo katika jamii zetu za leo. Dakta Yazdani, Mhadhiri katika vyuo vikuu vya Iran anasema kwamba hakika ya Mwenyezi Mungu iko wazi kwa watu wote bila ya kubanwa kwa kundi maalumu la watu.

Anasema kuwa njia za mwongozo wa kidini pia ni za kimantiki na kiakili ambazo zinaweza kufahamika na kila mtu. Anaongeza kuwa, mafundisho ya kidini yanaweza kutekelezwa kikamilifu katika jamii bila ya matizo yoyote, jambo ambalo anasisitiza kuwa linaonekana wazi katika sera na maisha ya Mtume katika uongozi wake wa jamii. Anasema kuwa Mtume aliweza kuongoza matabaka tofauti ya jamii bila ya kumdhulumu mtu yoyote katika matabaka hayo. Alikuwa akiipa akili thamani na umuhimu mkubwa katika jamii.

Mhadhiri Yazdani anamaliza kwa kusema kuwa Mtume alikuwa akizingatia kwa kina hali na mazingira tofauti yaliyokuwa yakitawala katika zama zake na kuyachukulia mashauriano na watu kuwa nguzo muhimu ya serikali yake. Wataalamu wengi wa masuala ya historia na dini wanaamini kwamba sifa muhimu ya serikali ya Mtume Muhammad (SAW) ni fadhila na maadili yake bora. Muelekeo mzima wa maisha ya kisiasa ya Mtume Muhammad (SAW) ulizingatia utukufu na ustawi wa kimaada na kimaanawi wa mwanadamu. Sifa muhimu za maadili na akhlaqi bora ya Mtume zilidhihirika wazi katika rehema, usamehevu, ukakamavu na ushujaa wake katika kutetea haki na uadilifu. Jambo hilo linaonekana wazi katika barua za kisiasa alizokuwa akiziandika Mtume ambapo masuala ya suluhu na urafiki, mafundisho ya maadili, uadilifu na mahaba yanadhihiri wazi katika barua hizo.

Dakta Muhammad Sutudeh, mwanachama wa jopo la kielimu katika mojawapo ya vyuo vikuu vya Iran anasema hivi kuhusu jambo hilo: " Katika hati ya Madina, Mtume Mtukufu alibainisha wazi jinsi watu wanavyopasa kuamiliana wao kwa wao na jinsi wanavyopasa kuamiliana na serikali ya Kiislamu na hivyo kuweka wazi uwezo na nguvu ya serikali. Hatua za kifikra, kiutamaduni, kiuchumi na kiulinzi za Mtume Mtukufu (SAW) katika kubuni serikali mpya, zinabainisha wazi juhudi kubwa alizofanya katika kuimarisha uwezo na mshikamano wa umma wa Kiislamu. Mtume daima alikuwa kifanya juhudi za kubuni jamii iliyo na utulivu na uthabiti wa kutosha. Jombo hilo pekee lilitosha kuimarisha uwezo wa harakati na udiplomasia wa Mtume katika uwanja wa siasa za nje pamoja na uwezo wake wa kukabiliana na wapinzani na maadui wa Uislamu."

Mtume aliimarisha zaidi wito na ulinganiaji wake wa kidini kwa kuwaandikia barua watawala wa mataifa kadhaa katika zama zake. Uzingatiaji wa kina na wa kiuadilifu wa serikali ya Mtume mjini Madina unabainisha wazi kwamba dini yake ilikuwa ni dini ya amani na urafiki. Mtume Mtukufu (SAW) hata alikuwa akihuzunishwa mno na hatua ya baadhi ya watu ya kuacha njia ya saada na wongofu na kuzama kwenye maovu na akiwaombea pamoja na kujaribu kuwarudisha kwenye njia nyoofu na ya wongofu. Alikuwa shakhsia adhimu, ambapo utukufu wa Uislamu unatokana na juhudi zake kubwa alizofanya kwa ikhalisi na uaminifu mkubwa kwa Mwenyezi Mungu. Utekelezwaji uadilifu na kuondoa ubaguzi ndilo jambo kubwa zaidi lililokuwa likimshughulisha Mtume katika kushughulikia masuala ya jamii na serikali.

Uadilifu ni msingi muhimu katika uthabiti wa jamii. Mtume alitumia uwezo wake wote kuhakikisha kwamba anatekeleza na kueneza uadilifu katika sehemu zote za jamii. Mtume hukutoa fursa maalumu wala kuwapendelea watu fulani waliojiona kuwa bora kuliko wenzao kwenye jamii. Aliwachukulia watu wote kuwa sawa mbele ya sheria katika serikali yake. Watu walivutiwa sana na utendaji na sheria za serikali yake na hivyo kufurahia uadilifu uliokuwa ukitekelezwa. Suala hilo liliwapelekea kuhisi kuwa na mustkabali mwema maishani. Goteh mshairi na mwandishi wa Ujerumani alivutiwa sana na Mtume Muhammad (SAW) kutokana na athari kubwa aliyoacha katika jamii ya mwanadamu duniani, Anamtambua Mtume Muhammad kuwa kiongozi wa kimaanawi wa jamii ya mwanadamu. Kwa mara nyingine tena tunawapongeza Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu adhimu wa kuzaliwa Mtukufu Mtume (SAW).

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top