0
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam.
Image result for philip mpango
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa Serikali imeanza kuyafanyia kazi maoni na malalamiko ya wafanyabiashara na wawekezaji kwa ujumla kuhusu kodi zinazolalamikwa kwa lengo la kuhuisha ama kubadili kodi zinazoonekana kuwa ni kero
Dkt Mpango amesema hayo mara baada ya kutembelea na kukagua maonesho ya kwanza ya viwanda vya ndani, yanayofanyika katika Uwanja wa maonesho ya biashara wa Mwalimu J. K. Nyerere, barabara ya Kilwa, Jijini Dar es salaam.
Amewataka wafanyabiashara na wawekezaji kuwasilisha maoni yao kuanzia mwezi huu wa Desemba wakati ambapo Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, iko katika mchakato wa kuandaa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2017/2018.
Hata hivyo amewataka watanzania na wafanyabiashara kwa ujumla kujenga utamaduni wa kulipa kodi ili kuijengea uwezo serikali wa kuwahudumia katika nyanja mbalimbali za maendeleo na huduma za jamii
Wakati huo huo, Dkt. Mpango, amewataka watanzania kujenga tabia na utamaduni wa kuthamini na kununua bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini ili kujenga uchumi wa ndani badala ya kununua vitu kutoka nje ya nchi ambavyo vingi kwa sasa vinazidiwa ubora na bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini.
Zaidi ya wafanyabiashara 400 wamejitokeza kushiriki katika maonesho ya kwanza ya viwanda vya ndani yanayotarajiwa kufungwa leo katika uwanja wa maonesho ya biashara wa mwalimu J.K Nyerere, barabra ya Kilwa, Dar es salaam, ambapo maonesho hayo yameelezwa kuwa na mafanikio makubwa.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top