Benny Mwaipaja-WFM, Dodoma
SERIKALI
imesema kuwa Benki Kuu ya Tanzania haina mamlaka kisheria ya kuweka
ukomo wa riba au riba elekezi itakayotumiwa na taasisi za fedha nchini
zikiwemo benki katika kutoa mikopo.
Kauli
hiyo imetolewa Bungeni mjini Dodoma, Februari 3, 2017 na Naibu Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akijibu maswali ya
msingi yaliyoulizwa na Mbunge wa Jimbo la Mbagala, Mhe. Issa Ali
Mangungu, aliyetaka kujua kama serikali inaweza kuandaa utaratibu
maalumu wa riba elekezi itakayowawezesha wanawake na vijana kupata
mikopo kwenye benki kwa riba nafuu ili waweze kujikwamua kiuchumi
Aidha
Mbunge huyo alitaka kufahamu kama Serikali inaweza kuziagiza benki za
biashara kulegeza masharti ya dhamana kwa vijana na wanawake ambayo
amedai yanarefusha mchakato wa upatikanaji wa mikopo kwa makundi hayo.
Dkt.
Kijaji amesema kuwa viwango vya riba katika benki na taasisi nyingine
za fedha hupangwa na taasisi husika kwa kutegemea mambo mengi ikiwemo
nguvu ya soko, sifa za mkopaji, ushindani katika soko, gharama za
upatikanaji wa fedha, mwenendo wa riba za dhamana za serikali, gharama
za uendeshaji na matarajio ya mfumuko wa bei.
Amesema
kuwa Benki Kuu imepewa mamlaka kisheria kusimamia Benki na Taasissi
nyingine za fedha hivyo haiwezi kuingilia upangaji wa riba za mikopo
kwenye taasisi hizo kwakuwa jambo hilo linapingana na mfumo wa uchumi wa
soko huria.
“Kutoa
maelekezo kwa benki na taasisi za fedha kutumia viwango fulani vya riba
katika biashara zao, kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya
kuzichukulia hatua endapo zitapata hasara kwa kutumia riba iliyopangwa
ama kuelekezwa na Benki Kuu” alisisitiza Dkt. Kijaji
Naibu
Waziri huyo wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa Benki
Kuu imeendelea na jukumu lake la msingi la kuhakikisha kuwa mfumo huo
unaendeshwa kwa kuzingatia sheria zilizowekwa ili kulinda maslahi ya
Taifa na uchumi kwa kusimamia ongezeko la ujazi wa fedha ili kuhakikisha
linakwenda sambamba na mahitaji halisi ya uchumi ili kudhibiti mfumuko
wa bei.
Ameyataja
majukumu mengine ya BOT kuwa ni kuhakikisha kuwa ongezeko la mikopo ya
benki haliathiri uzalishaji mali kulingana na malengo ya ujazi wa fedha,
kuhakikisha kuwa soko la dhamana la serikali linaendeshwa kwa ufanisi
ili liweze kutoa riba elekezi kulingana na hali ya soko na uchumi kwa
ujumla.
Post a Comment
karibu kwa maoni