Kamati
ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imekosoa utaratibu wa Serikali
kuhamisha baadhi ya walimu wa shule za sekondari kufundisha shule za
msingi kwa maelezo kuwa kila ngazi ya ualimu ina miongozo na mafunzo
yake mahsusi.
Akiwasilisha
maoni ya kamati hiyo kuhusu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
mwaka 2018/19 kwa niaba ya mwenyekiti, Peter Serukamba, mbunge wa Nzega
Mjini, Hussein Bashe amesema Serikali inatakiwa kuliangalia suala hilo
kwa jicho la pekee.
“Kamati
inatambua na kuelewa tatizo la ukosefu wa walimu hasa katika shule za
msingi hapa nchini, ila kuchukua walimu wa sekondari kwenda kufundisha
shule za msingi si sawa,” amesema Bashe.
Mbunge huyo ameyasema hayo leo Aprili 30 bungeni mjini Dodoma.
“Kumchukua
mwalimu wa sekondari kwenda kufundisha shule ya msingi kumepokelewa kwa
hisia tofauti miongoni mwa jamii na walimu wenyewe ikiwemo kuhisi
kuadhibiwa hivyo kushusha morali ya kufanya kazi.”
Amesema
Serikali inapaswa kutazama uamuzi huo kwa jicho la pekee na kufanya
uamuzi ulio sahihi kwa mustakabali mzuri wa elimu nchini.
Pia,
amesema kamati hiyo ina taarifa kuwa mahitaji ya walimu kwa shule za
msingi ni 273,454 lakini walimu waliopo ni 175,946 na hivyo kuwa na
upungufu wa walimu 97,508 sawa na asilimia 35.
“Kwa
shule za sekondari hasa masomo ya sayansi, mahitaji ni walimu 35,136
lakini waliopo ni 19,285 na hivyo kuwa na upungufu wa walimu 15,851 sawa
na asilimia 45.1,” amesema Bashe.
Post a Comment
karibu kwa maoni