Watu
wanne wakiwamo watatu wa familia moja, wamefariki dunia baada ya nyumba
zao kusombwa na mafuriko kutokana na mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia
jana katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.
Hata hivyo, viongozi mbalimbali wametoa takwimu zinazotofautiana kuhusu idadi ya vifo vilivyotokea.
Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema watu wanane walikuwa
wameripotiwa kufariki dunia na kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa
ilikuwa inajiandaa kwenda eneo la tukio ili kujionea uharibifu
uliotokea.
Lakini,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema taarifa
alizonazo ni za watu watatu waliopoteza maisha na kwamba bado hajapata
taarifa sahihi za tukio ambalo lilitokea katika vijiji vya Mang’angu na
Chinyika katika Kata ya Ving’awe.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, mmoja wa manusura, Beka Mlami (10) alisema
walikuwa wamelala wakiwa watano katika nyumba yao mvua kubwa ilipoanza
kunyesha kuanzia saa tatu usiku na ilipofika usiku wa manane nyumba yao
iliyojengwa kwa udongo ilisombwa na maji.
Mbali
na yeye, wengine waliokuwa katika nyumba hiyo ni Martha Sumisumi (60),
Shukuru Donald (15) aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika
Shule ya Sekondari Mwanakianga, Bernadetha Sumisumi (9) aliyekuwa
mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Ilolo na Joseph
Sumisumi (12) ambaye alinusurika.
Beka
alisema baada ya kuona maji yameingia ndani, aliwaambia ndugu zake
wakimbie watoke nje na wakati wanajiandaa kuvaa nguo nyumba yao
ilianguka na kuwaponda, lakini yeye alifanikiwa kutoka na kupanda juu ya
bati.
Alisema
baada ya kutoka nje ndipo gogo kubwa la mti lililosombwa na maji
lilipopiga nyumba yao na kuanguka chini hivyo ndugu zake wengine
kushindwa kutoka na hivyo kusombwa na maji.
Alisema baada ya kutoka nje alimwona ndugu yake mwingine Joseph akiwa anapelekwa na maji, lakini alifanikiwa kujiokoa.
Mkazi
mwingine wa eneo hilo, Steven Noel alisema nyumba iliyosombwa na maji
ilikuwa imejengwa karibu na korongo la maji, hivyo baada ya mvua
kunyesha, maji yaliacha mkondo wake na kuingia kwenye makazi ya watu na
kusababisha maafa hayo.
“Mvua
ilisababisha mafuriko makubwa ambayo yalikuwa yamebeba na magogo
makubwa ambayo yaliipiga ile nyumba na kuivunja katikati,” alisema Noel.
Alisema
baada ya gogo la mti kuipiga nyumba hiyo, maji yalijaa ndani na kwa
kuwa milango ilikuwa imefungwa, yalikosa njia ya kutokea na kuiangusha.
Noel
alisema kulipopambazuka, walifukua na kuipata miili ya watu hao watatu
huku mwili mwingine wa Jesca Lubeleje (19) mkazi wa Kijiji cha Chinyika
ukiokotwa.
Post a Comment
karibu kwa maoni