Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Waziri wa Fedha na Mipango ameishukuru Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB) kwa kukubali kuendelea kufadhili miradi ya maendeleo ya
kipaumbele hususani ya ujenzi wa barabara na usafirishaji wa umeme ili kufungua
fursa za kiuchumi katika kanda ya Magharibi.
Dkt. Mpango ametoa shukrani hizo alipokutana na Wakurugenzi
Watendaji 12 wanaowakilisha nchi zao katika Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB), jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) ameiomba
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kuharakisha kazi za upembuzi yakinifu na
hatimaye kutoa fedha ili utekelezaji wa miradi ya Maendeleo kuanza mapema iwezekanavyo.
Amesema kuwa Benki hiyo iliahidi kutoa fedha ili kujenga barabara
ya Nyakanazi, kupitia Kibondo, Kasulu hadi Manyovu, kwa kiwango cha lami na
kwamba mradi huo ukipatiwa fedha na kukamilika kwa wakati kutasaidia kuchochea
biashara ya wakazi wa maeneo hayo na Nchi jirani ya Burundi.
Pia mradi wa North – West grid wa kusafirisha Nishati ya Umeme
kutoka Shinyanga hadi Mbeya kupitia Kigoma Katavi na Rukwa. Mradi huu
utawezesha Mikoa ya ukanda wa Magharibi kupata Nishati ya uhakika ya umeme na
kufungua fursa za Maendeleo mbalimbali yakiwemo ya ujenzi wa Viwanda vidogo na vya kati.
“Katika kikao hicho tumewaeleza Wakurugenzi hao wa AfDB hatua
mbalimbali ambazo Serikali inazichukua katika kutatua changamoto ya Miundombinu
ya Umeme na Barabara, kupanua fursa za Ajira, na kuharakisha maendeleo ya ukuaji wa Sekta ya Kilimo ambayo inategemewa
na wananchi wengi” Alifafanua Waziri Mpango.
Aidha amewaeleza wageni juu ya jitihada za Serikali ya Mhe. Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli za kukusanya
mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, kupambana na rushwa na biashara haramu ya
madawa ya kulevya.
Waziri Mpango ametumia fursa hiyo kuomba AfDB kusaidia kujenga
uwezo wa Tanzania kukabiliana na majanga yakiwemo ya matetemeko ya ardhi, ajali
kubwa za majini na kwenye migodi. Maeneo mengine ambayo AfDB imeombwa kuisaidia
Tanzania ni uvunaji wa rasilimali za bahari (blue economy), kuelekeza mitaji
katika Sekta ya kilimo na kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabia nchi.
Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)
ameipongeza Benki ya AfDB kwa kuwa mdau mkubwa wa Maendeleo ya nchi za Afrika
na hasa Tanzania kwa kuwa imekuwa mnufaika mkubwa wa program/ miradi
inayofadhiliwa na Benki hiyo.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wageni hao watakapokuwa
wakitembelea miradi mbalimbali inayogharamiwa na AfDBi katika siku takribani
tano ambazo watakuwepo nchini.
Kwa upande wa Wakurugenzi Watendaji wa AfDB wanaoziwakilisha nchi
zao, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji kutoka Afrika ya Kusini Bi. Elizabeth
Mmakgoshilekethe, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa mafanikio ya
kiuchumi kwa kuwa Tanzania imekuwa na viashiria vingi ambavyo vinaonesha uchumi
wa Taifa ni imara ukilinganisha na nchi nyingine katika bara la Afrika kusini
mwa jangwa la Sahara.
Aidha wameitaka Tanzania kuendeleza jitihada za kupambana na
Umaskini hasa katika maeneo ya vijijini na kuongeza fursa za ajira ili
kuharakisha maendeleo. Pia wameipongeza Serikali kwa mikakati waliyonayo kupitia
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka
mitano kwa kuwa unaendana na vipaumbele vya Benki hiyo.
Benki hiyo imeitaka pia Tanzania kushiriki na kuchangamkia fursa
za miradi ya kikanda hasa katika Nishati ya Umeme, Barabara na Reli na pia
kuhakikisha utawala bora.
Post a Comment
karibu kwa maoni