Ankal
Issa Michuzi wa Michuzi TV, Millard Ayo na Askofu wa Ayo TV na Abdallah Mrisho
wa Global TV wakitoka makao makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano walikoitwa kuchukua
barua zao zinazowazuia kuendelea kutoa huduma za TV mtandao hadi hapo kanuni za
usajili na leseni utapokamilika.
|
Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezitaka Michuzi TV, AYO TV na Global TV kusitisha
huduma zao za TV mtandaoni hadi hapo kanuni za usajili rasmi ambazo mamlaka
hiyo imesema inaandaa kwa huduma hizo zitapokuwa tayari.
Barua hiyo,
iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu Mhandisi James Kilaba tarehe 30 January mwaka
huu, imevitaka vyombo hivyo ambavyo vinapendwa sana nchini na nje ya nchi
kuacha mara moja kutoa huduma za TV mtandaoni.
"Kwa
mujibu wa section 13 (1) of the electronic and postal communications Act Cap
306, sheria za Tanzania zinahitaji watoa huduma zozote za aina hiyo wanahitaji
leseni kutoka mamlaka ya mawasiliano", imesema barua hiyo.
Wamiliki wa
mitandao hiyo - Millard Ayo, Ankal Issa Michuzi na Abdallah Mrisho - wameeleza
kushtushwa kwao kwa agizo hilo la ghafla, tena wakati hata kanuni zenyewe
hazijawekwa.
"Gloval
TV ipo tayari hata leo kukamilisha taratibu za usajili - kama zingekuwepo - na
kwa sababu bado kukamilika tunaomba kupewa muda zaidi chini ya uangalizi wakati
tunasubiria kanuni hizo mpya," alisema Abdallah Mrisho, Meneja Mkuu wa
Global Publishers.
Ankal
Michuzi na Millard Ayo waliunga mkono kauli hiyo na kwa pamoja watatu hao
wameomba kuonana na mkurugenzi wa TCRA ili kuwasilisha maombi rasmi ya
kuruhisiwa kuendelea kutoa huduma hiyo kwa muda wakati kanuni
zikisubiriwa.
Bahati mbaya
Mhandisi Kilaba alikuwa safari na swala hilo limepangwa kushughuliwa ataporejea
wiki ijayo.
"Ukizingatia
kwamba tumekuwa tunatoa huduma hii kwa muda mrefu na haijulikani kanuni
zitakuwa tayari lini tunaomba TCRA iangalie namna ya kufanya ili wananchi
wanaotutegemea sana wasikose huduma hii", alisema Ankal.
Hata
hivyo vituo hivyo vitatu vinaendelea kuhudumu nje ya mchakato wa TV mtandao.
Ayo TV,
Michuzi TV na Global TV, ambazo zinaongoza kwa mbali kwa kutazamwa na
watu wengi nchini na nje ya nchi, ni TV mtandao pekee zilizoitikia mwito wa
TCRA, kati ya vituo mtandao takriban 51 vilivyopata barua hiyo.
Post a Comment
karibu kwa maoni