Kichanga chenye umri usiozidi wiki moja ambacho hakikufahamika jina lake, kilitelekezwa katika nyumba ya kulala wageni inayojulikana kwa jina la Kibara, iliyopo Musoma Mjini Ijumaa iliyopita
Kwa mujibu wa ofisa mmoja wa Ustawi wa Jamii katika Hospitali ya Mkoa wa Musoma, aliyejulikana kwa jina moja Clavery, kichanga hicho kilitelekezwa na mama yake mzazi, aliyefika katika gesti hiyo akiwa na watoto wake wawili, mmoja mkubwa akiwa na umri unaokadiriwa kuwa miaka miwili.
Alisema alipopanga katika nyumba hiyo, alikaa kwa muda kabla ya kumuomba mhudumu wa nyumba hiyo, amuangalizie mtoto wake huyo, wakati yeye akienda kutafuta chakula kwa ajili ya mtoto mkubwa, mfanyakazi huyo hakuwa na kipingamizi.
Mama Msamalia mwema akimbeba mtoto huyo.
“Sasa akiwa anaendelea na shughuli zake, mara akasikia mtoto huyo mchanga analia, akajua ni jambo la kawaida na mzazi wake atarudi mapema, lakini muda ukazidi kwenda na hakutokea, akalazimika kuwaita akina mama majirani ndipo waliamua kwenda kutoa taarifa polisi,” alisema ofisa huyo.
“Akina mama hao waliokuwa wakimgombea ili kumtazama mtoto, hawakuamini kama mama anaweza kumtelekeza mtoto wake wa kumzaa, wakamchunguza kama ana ulemavu wowote, lakini wakamkuta mzima, ndipo wakampeleka polisi,” alisema.
Baada ya kufika kituo cha polisi na kutoa taarifa hizo, askari hao walimpeleka mtoto huyo hospitalini, ambako alipokelewa na kuanza kuangaliwa tangu siku hiyo hadi leo na mama yake hajulikani alipo.
“Alipoletwa hapa alikuwa katika hali mbaya, tumejaribu kumhudumia kwa kadiri tunavyoweza na hali yake inaendelea vizuri, hii siyo mara ya kwanza kukutana na kesi kama hizi, mwaka jana kuna mwingine aliletwa hapa naye akitorokwa na mama yake, hatukuwa tukilijua jina lake, tukaamua kumuita Eliah.
“Sasa na huyu naye ameletwa na jina lake hatulijui, kwa hiyo sisi hapa tumeamua kumwita jina la Elisha, kwa kuwa ni wa kiume, tutaendelea kuwa naye hadi hapo baadaye uamuzi mwingine utakapochukuliwa na serikali,” alisema Clavery, aliyedai kukaimu nafasi ya ofisa ustawi katika hospitali hiyo.
Jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhan Ng’azi hazikuzaa matunda kwani simu yake ya kiganjani haikupokelewa kila ilipopigwa.
Post a Comment
karibu kwa maoni