0
MWALIMU Mkuu wa shule ya msingi, kijiji cha Kilimanjaro mkoani Lindi, anadaiwa kukatisha masomo ya mwanafunzi wake wa darasa la sita (jina linahifadhiwa) kwa madai ya kumpa ujauzito. 

Akizungumza na timu ya waandishi waliotembelea kijijini hapo juzi, mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 16, alidai kuwa alikuwa akipewa vitisho na mwalimu huyo kama angeshindwa kutekeleza matakwa yake.

“Mwalimu (akimtaja jina) baada ya kunieleza kile anachokitaka kwangu, nilipomkatalia alianza kunifanyia vituko, ikiwamo kunichapa viboko na kudai atanifukuza shule akidai sina akili darasani na nawasumbua walimu,” alisema.

Alisema kutokana na visa alivyokuwa akifanyiwa na mwalimu mkuu huyo, alilazimika kutekeleza matakwa yake, akifikiri ni moja ya njia ya kujiokoa na visa alivyokuwa akifanyiwa ili asifukuzwe shule, hatimaye akajikuta akipata ujauzito asioutegemea.

Mwanafunzi huyo ambaye ana ujauzito wa miezi tisa, alisema baada ya mwalimu huyo kubaini mabadiliko, alimpa vitisho vingine, ikiwamo kuwafunga jela wazazi wake, iwapo atamtaja kuwa ndiye aliyempa ujauzito huo.

“Kutokana na kauli hiyo ya mwalimu wangu, niliendelea kuogopa kumtaja hata pale, wazazi waliponitaka niwatajie mwanaume mwenye mzigo huu,” alidai.

Alisema walipofikishwa kituo cha polisi, akalazimika kuvunja ukimya na kumtaja mwalimu wake kuwa ndiye aliyempa ujauzito huo.

Mama mzazi wa mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa), alisema kutokana na homa za mara kwa mara anazozipata binti huyo alimuhoji bila ya mafanikio, kisha kuamua kumpeleka zahanati na kubainika kuwa ana ujauzito.

Baba mzazi wa mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa), aliwaambia waandishi hao kuwa kitendo cha binti yake kutoudhuria shule, ndicho kilichomfanya amhoji na kukosa maelezo na kuamua kuonana na uongozi wa shule hata hivyo, alidai hakupata ushirikiano.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Rashidi Said Kulakwenda, alipoulizwa juu ya madai hayo, alisema Ofisi yake haijapokea malalamiko kutoka kwa mzazi huyo, huku taarifa za kupewa mimba kwa mwanafunzi na mwalimu wake akidai kuzipata kupitia kwa wananchi.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo, alimuita mwalimu huyo ofisini kwake zaidi ya mara nne bila ya mafanikio, kwa madai ya kukabiliwa na majukumu.

Mwalimu mkuu huyo alipofuatwa ili kupata kauli yake, alikataa kuelezea suala hilo, akidai lipo mikononi mwa polisi na kusema mwanaume aliyempa mimba mwanafunzi huyo amekamatwa kwa mahojiano.

Kamanda wa Polisi mkoani Lindi ACP Renatha Mzinga, aliamua kuitisha faili kabla ya kwenda kwa mwanasheria wa mkoa kwa ajili ya kupelekwa mahakamani na kuomba wampe nafasi kulipitia.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top