0
Na Benny Mwaipaja, WFM

Displaying IMG_8914.JPG
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji kutoka Afrika ya Kusini Bi. Mmakgoshi Lekhethe (kulia) wakipeana mikono baada ya kumalizika kwa mkutano wa tathmini ya maendeleo ya Miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo nchini Tanzania, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema Serikali inaendelea kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika kuhakikisha miradi yote ikiwemo ile inayofadhiliwa na Benki hiyo inatekelezeka kwa ufanisi Mkubwa.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo alipokutana na Wakurugenzi Watendaji 12 wanaoziwakilisha nchi zao katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), katika Mkutano uliofanyika Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es salaam, baada ya ujumbe huo kutembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Benki hiyo hapa nchini.
Displaying IMG_8921.JPG
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wanne kulia) na Mkurugenzi Mtendaji kutoka Afrika ya Kusini Bi. Mmakgoshi Lekhethe (wa tano kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi Watendaji wanao ziwakilisha nchi zao katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), baada ya kumalizika kwa mkutano wa tathmini ya maendeleo ya Miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo nchini Tanzania, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
“Madhumuni makubwa ya ziara ya Wakurugenzi watendaji wa Benki ya AfDB  waliokuja nchini tangu Februari 25, ni kukaa pamoja na Serikali ili kujadiliana kuhusu sera  na mipango mikakati ya maendeleo, lakini pia  kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa kupitia ufadhili wa Benki ya hiyo” Alifafanua Dkt. Kijaji.
Wakurugenzi hao ambao ndio watoa maamuzi katika Benki hiyo, wametembelea miradi ya maji Zanzibar na kwa upande wa Tanzania Bara wametembelea mradi wa kufua umeme wa Sokoine substation uliopo Manispaa ya Ilala.
Katika Mkutano huo, Serikali ya Tanzania imeendelea kuiomba Benki ya AfDB  kuharakisha kazi za upembuzi yakinifu na hatimaye kutoa fedha ili utekelezaji wa miradi ya Maendeleo uanze mapema kwa kadri inavyowezekana.
Miradi hiyo ni pamoja na ule wa North – West grid wa kusafirisha Nishati ya Umeme kutoka Shinyanga hadi Mbeya kupitia Kigoma Katavi na Rukwa. Mradi utakaowezesha Mikoa ya Ukanda wa Magharibi kupata Nishati ya uhakika ya umeme na kufungua fursa za Maendeleo mbalimbali yakiwemo ya ujenzi wa Viwanda vidogo na vya kati.
Kwa kushirikiana na Benki hiyo ya AfDB mradi mwingine unaofanyiwa kazi ili kupata fedha za kuanza kuutekeleza ni ule wa  kujenga barabara ya Nyakanazi, kupitia Kibondo, Kasulu hadi Manyovu, kwa kiwango cha lami na iwapo mradi huo ukipatiwa fedha na kukamilika kwa wakati kutasaidia kuchochea biashara ya wakazi wa maeneo hayo pamoja na  Nchi ya Burundi.
Kwa upande wa Wakurugenzi Watendaji wa AfDB wanaoziwakilisha nchi zao, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji kutoka Afrika ya Kusini Bi. Mmakgoshi Lekhethe, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Joseph Magufuli kwa ufanisi katika Nyanja zote ikiwemo ya kupambana na umaskini.
Wageni hao wamefurahishwa na namna Tanzania invyotekeleza miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo, kwa kuwa kila walipopatembelea, wameona uthabiti na umadhubuti wa miradi, jambo ambalo limewaongezea hamasa ya kufanya kazi kwa karibu na nchi hiyo.
Wameitaka Serikali kuendelea kulishughurikia suala la deni la Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania-TANESCO, ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji kwa lengo la kuchochea maendeleo ya nchi mijini na Vijijini.
Naibu Waziri Dkt. Kijaji amebainisha kuwa ipo mikakati iliyowekwa na Serikali ya kutatua suala la deni hilo kwa kuwa tatizo kubwa lilikuwa matumizi ya Mafuta ya dizeli katika kuendeshea mitambo TANESCO.
Aidha alisema kuwa kwa sasa upatikanaji wa Nishati ya Gesi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, utasaidia katika kuendesha mitambo hiyo badala ya Mafuta hivyo kutatua suala la deni hilo linalo likabili Shirika na hatimaye kutimiza ndoto ya watanzania ya kuimarika kwa uchumi utakao chochewa na Sekta hiyo.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top