0
Na Benny Mwaipaja, WFM-Morogoro
Displaying IMG_8145.JPGWatumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango nchini wametakiwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuiletea nchi Maendeleo ya haraka kupitia falsafa ya uchumi wa viwanda utakao iwezesha nchi kuwa ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kusimamia matumizi yake ipasavyo.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Dorothy Mwanyika, wakati akifungua mkutano wa 13 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo unaofanyika mjini Morogoro kwa siku mbili.
Bi. Mwanyika  amesema kuwa Mabaraza ya wafanyakazi sehemu za kazi, yana malengo ya  kuongeza tija, ufanisi na ushirikishwaji wa wafanyakazi  katika uongozi wa pamoja mahali pa kazi kama agizo la Rais Na. 1 la mwaka 1970 likisomwa pamoja na miongozo mingine linavyo elekeza.  
Aidha amewataka wajumbe wa Baraza hilo kukumbuka maelekezo ya viongozi wakuu wa nchi wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, kuhusu kusimamia ukusanyaji wa mapato na nidhamu ya matumizi ya Fedha za Umma, ili kujenga uchumi wa Viwanda na kufikia maendeleo stahiki.
“Tuunge mkono juhudi za Serikali kwa kutafsri maelekezo ya viongozi kwa vitendo ili kuthibitisha msemo usemao Wizara ya Fedha na Mipango ndiyo moyo wa Serikali” alisisitiza Bi. Mwanyika.
Pia Bi. Mwanyika amewashukuru viongozi wa Wizara hiyo kwa kufanikisha mpango wa Serikali wa kuhamia Dodoma ambapo katika awamu ya kwanza wafanyakazi 184 wameripoti mkoani humo licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa makazi.  Hata hivyo amewataka watumishi hao kushirikiana katika kutatua changamoto hizo kwa pamoja.
Kwa upande wake Katibu wa Baraza  la Wafanyakazi wa Wizara hiyo Bw. Cyprian Kuyava, amebainisha mafanikio yaliyopatikana  kutokana na maazimio mbalimbali ya Mkutano uliopita wa mwaka  2015/2016 kuwa ni pamoja na kuboresha huduma kwa watumishi, kuboresha mazingira ya kazi na kuongezeka kwa mshikamano miongoni mwa wafanyakazi licha ya ufinyu wa Bajeti.
Naye Mkurugenzi wa huduma za Sheria wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi Susana Mkapa amesema Watumishi wa Wizara hiyo wako tayari kuunga mkono juhudi za Serikali za ukusanyaji wa mapato, kubana matumizi na hatua ya Serikali kuhamia Dodoma.

Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha unafanyika kwa siku mbili kuanzia Machi 27 hadi 28, 2017, huku ajenda kuu ikiwa kufanya mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2016/2017 na kujadili makadirio ya bajeti ya mwaka 2017/2018.  

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top