Benny Mwaipaja,
WFM-Dodoma
Benki ya Taifa ya
Biashara (NBC) kwa mara ya kwanza imetoa gawiwo la shilingi bilioni 1.7 kwa
Serikali ambayo inamiliki asilimia 30 ya hisa za Benki hiyo.
Hundi kifani ya
kiasi hicho cha fedha alikabidhiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip
Mpango (Mb), kwaniaba ya Waziri Mkuu, katika tukio la Benki hiyo kuadhimisha
miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, tukio lililofanyika katika Hoteli ya Morena
Mjini Dodoma.
Hii itakuwa mara ya
kwanza kwa Benki hiyo kutoa gawiwo kwa wanahisa wake katika kipindi cha miaka 9
baada ya kuanza kupata faida ya uwekezaji wake hapa nchini.
Dkt. Mpango
aliishukuru Benki hiyo kwa kuanza kutoa gawiwo kwa wanahisa wake baada ya ukame
wa muda mrefu na kuelezea matumaini yake kwamba kiasi cha gawiwo kitaongezeka
zaidi miaka ijayo.
Hata hivyo alizitaka
Benki zote hapa nchini kupunguza riba za mikopo inazotoza kwa wateja wao hasa
baada ya Benki Kuu ya Tanzania-BOT kupunguza riba za mikopo kwa mabenki kutoka
asilimia 16 hadi asilimia 12.
Alizitaka pia taasisi
za fedha nchini, kuwekeza fedha katika kutekeleza Mpango wa Pili wa Taifa wa
Maendeleo kwa njia ya mikopo kwa wateja wao kwa ajili ya ujenzi wa viwanda
vitakavyosisimua uchumi na kukuza ajira nchini.
Alipongeza pia
juhudi zilizofanywa na Benki hiyo kufanya uwekezaji mkubwa kwenye mtandao wa
malipo ya kielektroniki ikiwa ni maagizo ya Serikali kwamba malipo yote ya
Serikaloi yafanyike benki au kupitia miamala ya kielektroniki
“Nimefurahi kuthibitishiwa
kwamba, kutoka tarehe 1 Julai 2016 hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2017, NBC
imekusanya fedha za Serikali na kuzituma kielektroniki katika Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) jumla ya Shillingi Billioni 991” aliongeza Dkt. Mpango.
Mwenyekiti wa Bodi
ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Nehemiah Mchechu, alieleza Mkakati wa Benki hiyo
ya tatu kwa ukubwa hapa nchini ikitanguliwa na Benki za NMB na CRDB, huku ikiwa
imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 1, kwamba imejipanga kusogeza
huduma zake kwa wananchi na wafanyabiashara wa kati na wa chini kabisa.
“Mwaka jana Benki
yetu imepata faida ya zaidi ya shilingi bilioni 13 na katika mkutano Mkuu wa
wanahisa tuemekubaliana kutoa gawiwo kwa wawekezaji” aliongeza Bw. Mchechu.
NBC inamilikiwa na
wabia watatu, wakiwemo kundi la Mabenki ya Barclays (ABSA Group ltd) ya Afrika
Kusini, inayomiliki hisa nyingi zaidi, Serikali ya Tanzania yenye hisa asilimia
30 huku Benki ya Dunia kupitia Taasisi yake ya Fedha ijulikanayo kama The
International Finance Corporation (IFC), ikiwa na hisa asilimia 15.
Post a Comment
karibu kwa maoni