Watu
watatu ambao ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Butwa mkoani Geita
wamefariki dunia baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kuzama katika
Ziwa Victoria, mkoani Geita.
Kamanda
wa Polisi Mkoani Geita amesema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa
10 jioni wakati wanafunzi hao walipokuwa wakivuka maji kwa kutumia
mitumbwi miwili wakitoka shuleni katika kisiwa cha Isimacheli kurudi
majumbani kwao katika kisiwa cha Lulegea.
Amesema
wanafunzi hao jumla walikuwa 24 ambao walijigawa kwa kupanda wanafunzi
12 katika kila mtumbwi ambapo mtumbwi wa kwanza ulifanikiwa kuvuka
salama, lakini mtumbwi wa pili ulielemewa mawimbi na hatimaye kuzama.
Amesema
kwamba kabla mtumbwi huo haujazama, nahodha wa mtumbwi huo baada ya
kuona anaelemewa aliamua kurudi nyuma ili aurudishe ufukweni lakini
wakati akijaribu kurudi mtumbwi ulizidiwa na kuzama ambapo wanafunzi 9
wote wa kiume walinusurika baada ya kufanikiwa kuogelea huku watatu
ambao wote ni wa kike wakipoteza maisha.
Amewataja
waliofariki dunia kuwa ni pamoja na Kumbuka Bahati (13) mwanafunzi wa
darasa la 3, Anastazia Mwita mwanafunzi wa darasa la 3 na Sophia Lusala
mwanafunzi wa darasa la Kwanza.
Amesema mwili wa mwanafunzi mmoja ulipatikana jana majira ya jioni na miili miwili imepatikana leo ikiwa imeharibika vibaya
Jeshi hilo linamshikilia nahodha wa mtumbwi huo anayefahamika kwa jina la Hulugu Kayalenda na uchunguzi bado unaendelea.
Post a Comment
karibu kwa maoni