WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amezitaka benki mbalimbali nchini ikiwemo Benki ya
Maendeleo ya Kilimo kutoa mikopo kwa vikundi vya kilimo ili viweze
kupata fedha za kununulia matrekta.
Amesema Serikali imedhamiria kuimarisha Sekta ya kilimo ili kwenda sambamba na adhma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo jana Jumanne, Mei 23, 2017 wakati alipotembelea
kiwanda cha kuunganisha Matrekta URSUS-TAMCO, Kibaha mkoani Pwani.
Alisema
kiwanda hicho kinalenga kuboresha sekta ya kilimo nchini na kuongeza
uzalishaji wa malighafi za viwandani kwa kuwa wakulima watakuwa na zana
za kisasa.
Aidha,
amevitaka vyuo vya kilimo nchini kununua matrekta hayo kwa lengo la
kufundishia wanafunzi wake ili wanapohotimu wawe na uwezo wa kutumia
zana hizo vizuri na kwenda kuwasaidia wakulima katika maeneo yao.
Pia
Waziri Mkuu alitoa wito kwa Halmashauri nchini kuendelea kupanga
matumizi bora ya ardhi kwa kutenga maeneo ya kilimo, uwekezaji, makazi,
biashara na huduma za jamii, hivyo kuepuka migogoro ya ardhi kwa siku
zijazo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Bw.
Mlingi Mkucha alisema wataunganisha matrekta 2,400, harrow 2,400 na
majembe 2,400 katika mradi huo wa kiwanda cha kuunganisha matrekta
URSUS-TAMCO ikiwa ni mkataba wa awali.
Alisema
kiwanda hicho kina wafanyakazi 27 kwa hatua za mwanzo. Aidha, idadi
hiyo itaongezeka kutokana na mahitaji ambapo baadhi ya wafanyakazi
watapewa mafunzo nchini Poland na watakaporudi watakuwa wakufunzi wa
watakaoajiriwa.
Mkurugenzi
huyo aliongeza kuwa kiwanda hicho kimeazima wafanyakazi wengine
wakiwemo watano kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, 10 kutoka vyuo
mbalimbali vya ufundi nchini, wawili kutoka CAMARTEC ambao
wanashirikiana na wataalamu 10 kutoka URSUS kuunganisha matrekta.
Bw.
Mkucha alisema wafanyakazi 10 kutoka Tanzania wanatarajiwa kwenda
nchini Poland kufanya mafunzo mahsusi na watakaporejea watakuwa
wakufunzi kwa watumishi wengine watakaoajiriwa katika kiwanda hicho.
Alisema
mbali na ujenzi wa kiwanda hicho cha kuunganishia matrekta ya URSUS,
mradi unahusisha uanzishwaji wa vituo vinane kwa ajili ya kutoa huduma
kwa wateja na kuuzia matrekta, zana na vifaa vingine.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Everest Ndikilo alisema miongoni mwa
changamoto zinazoikabili sekta ya viwanda mkoani humo ni pamoja na
kukatika kwa umeme, hivyo ameliomba Shirika la Umeme Tanzania (TANECO)
kuongeza vituo vya kupozea umeme.
Awali
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mheshimiwa Charles Mwijage
alisema kwa sasa nchini kuna viwanda vikubwa 393 kati yake 84 viko
mkoani Pwani, ambapo amewaomba viongozi wa mkoa huo kutenga maeneo kwa
ajili ya wanawake na vijana kuanzisha viwanda vidogo.
Mara
baada ya kutembea kiwanda cha kuunganisha matrekta URSUS-TAMCO Waziri
Mkuu alitembelea eneo la uwekezaji la Kamal (Kamal Indusrial Estate)
lililoko katika Kata ya Kerege wilayani Bagamoyo.
Post a Comment
karibu kwa maoni