0
Jeshi la polisi mkoani Mwanza linawashikilia wanawake wawili katika matukio mawili tofauti likiwemo la mwanamke mmoja kumuua mwanaye.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema katika tukio la kwanza, mwanamke mmoja mkazi wa Kisiwa cha Nyamango, Kijiji cha Soswa katika Tarafa ya Buchosa, Nyamisi Bahati (27) anashikiliwa na polisi akituhumiwa kumuua mtoto wake, Sakimu Hassan mwenye umri wa miezi saba kwa kumtupa ndani ya Ziwa Victoria.

Msangi alisema tukio hilo lilitokea juzi saa moja usiku wakati mtuhumiwa alipotoka nyumbani kwake kwenda kuwasalimia wazazi wake huku ikidaiwa kuwa aliondoka akiwa na mtoto wake.

“Akiwa nyumbani kwao ghafla alitoka nje akiwa na mtoto wake, ilionekana kama anaenda kumbembeleza baada ya muda alirejea akiwa hana mtoto ndipo bibi yake alipoanza kuhoji alipo mtoto,” alisema Msangi.

Alisema baada ya kumhoji zaidi, baadaye mtuhumiwa alikiri kumtupa ndani ya Ziwa Victoria.

Baada ya bibi kupokea taarifa hiyo ilimshtua na kuanza kupiga kelele kuomba msaada kwa watu ili waweze kusaidia kumuokoa mtoto huyo.

Kamanda huyo aliendelea kueleza kuwa majirani waliokusanyika katika tukio hilo walisaidia kutoa taarifa kituo cha polisi ambao nao walifika eneo hilo na kuanza shughuli ya uokozi hadi walipofanikiwa kuupata mwili wa marehemu.

Msangi alisema uchunguzi wa awali umebainisha kuwa mtuhumiwa ana matatizo ya akili ingawa bado wapo kwenye upelelezi na mahojiano kujua ukweli wa jambo hilo.

Katika tukio la pili, polisi wanamshikilia mkazi wa mtaa wa Malulu, Kata ya Igogo wilayani Nyamagana, Ghati Chacha (36) kwa madai ya kukutwa na pombe haramu ya gongo lita 23.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top