Mvutano umeibuka bungeni kati ya mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.
Mvutano
huo umeibuka leo Mei 9, 2018 baada ya Mchungaji Msigwa kutakiwa kufuta
maneno aliyoyazungumza kuhusu utendaji wa Rais John Magufuli katika
mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji mwaka 2018/19.
Mbunge
huyo alianza kuzungumzia kero za maji majimboni, kueleza jinsi wabunge
wengi wanavyolalamikia jambo hilo na kubainisha kuwa kama ni suala la
uwajibikaji wa Serikali, inapaswa kuundwa tume.
Huku
akitolea mfano kukosekana kwa maji ni sawa na wananchi kula uchafu,
wakiwemo watalii na huenda wote wakapata ugonjwa wa kipindupindu,
Mchungaji Msigwa aliingia katika mvutano huo baada ya kudai kuwa tatizo
la maji ili litatuliwe ni mpaka Rais John Magufuli apige simu kwa Katibu
wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
“Yaani
tatizo la maji hadi Rais apige simu kwa katibu wa wizara, aunganishwe
na mtendaji wa kijiji, hii inaoyesha mfumo umekwama,” amesema.
Amesema katibu huyo wa wizara amejikita mitandaoni kujibizana na maaskofu badala ya kutafuta ufumbuzi wa maji.
Wakati
akiendelea kuchangia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista
Mhagama alisimama na kusema kwa mujibu wa kanuni ya 64, mbunge
hatozungumzia utendaji wa Rais ndani ya Bunge.
“Madaraka
aliyopewa Rais ni ya kikatiba, anaweza kusimamia jambo lolote, kwa
utaratibu wowote anaoona unafaa kwa muktadha wa Watanzania. Na kanuni
zinatufunza tusizungumzie mienendo ya Rais,” amesema Mhagama.
“Tukiacha
liendelee kama anavyofanya Mchungaji Msigwa si sawa na tunavunja
Katiba, ninaomba aheshimu kanuni ya 64 (1)(e) ya Bunge na kama
itakupendeza Naibu Spika hayo anayozungumza afute.”
Baada ya maelezo hayo, Naibu Spika alisimama na kumtaka Mchungaji Msigwa kufuta maneno hayo.
Hata
hivyo, Mchungaji Msigwa amesema hajui afute maneno gani jambo ambalo
lilimnyanyua tena Dk Tulia, “kama hujui ufute yapi, futa mchango wako
wote uliochangia na uanze moja.”
Agizo
hilo lilipingwa na Mchungaji Msigwa na kuendelea kuchangia kitendo
ambacho Dk Tulia hakukubaliana nacho na kumtaka aketi huku akimuita
mbunge mwingine kuendelea na mjadala wa bajeti ya wizara hiyo.
Post a Comment
karibu kwa maoni