Serikali imeeleza kuwa pamoja na
juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ikiwemo kutoa elimu juu ya uzazi wa
mpango, suala la udhibiti wa ongezeko la idadi ya watu nchini ni mtambuka
linalohitaji usimamizi na ushirikiano wa
wadau wote.
Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma
na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali
la Mbunge wa Kaliua Mhe. Magdalena Sakaya (CUF), aliyetaka kujua mpango wa
Serikali wa kudhibiti ongezeko la watu hapa nchini ili liendane na uwezo wa
Serikali wa kupeleka huduma muhimu kwa wananchi.
Dkt. Kijaji alisema kuwa, ongezeko
la idadi ya watu nchini inatokana na vizazi au idadi kubwa ya watoto ambao
akina mama wanazaa wakati wa uhai wao na ukosefu wa elimu kwa wasichana au
akina mama.
“Tafiti zinaonyesha kuwa akina mama
wenye elimu ya sekondari na kuendelea huzaa watoto wachache zaidi ikilinganishwa
na wanawake wasiokua na elimu” alieleza Dkt. Kijaji
Dkt. Kijaji aliongeza kuwa, Tanzania
ina Sera ya Idadi ya Watu iliyoridhiwa na Serikali mwaka 1992 lengo la sera
hiyo ni kupunguza kasi ya ongezeko la idadi ya watu ili kuhakikisha kuwa, idadi
yao inaendana na huduma za jamii zilizopo.
“Mambo yaliyobainishwa katika sera
hiyo ni namna Serikali ilivyojipanga kutoa elimu ya msingi na sekondari, usawa
kijinsia, umri wa kuolewa, matumizi ya njia za kisasa za uzazi na wajibu wa
kila mdau tukiwemo sisi Waheshimiwa Wabunge”. Alisema Dkt. Kijaji.
Aidha, alisema kuwa utafiti wa Afya ya Mama na
Mtoto ya mwaka 2015/2016 umeonesha kuwa endapo
mtoto wa kike atakaa shuleni kwa kipindi kirefu, uwezekano wa kuzaa
watoto wengi ni mdogo kwa vile elimu inamsaidia kujitambua na inampa uwezekano
mkubwa wa kujishughulisha na shughuli nyingine za kiuchumi na matumizi ya njia bora
ya uzazi wa mpango.
Katika swali la nyongeza Mbunge wa Kaliua
Mhe. Magdalena Sakaya, alihoji pamoja na kuwepo sera ya kudhibiti ongezeko la
watu nchini, bado katika maeneo ya vijijini watu wanazaa watoto wengi hali
inayo sababisha watoto kuishi katika mazingira magumu na kukosa huduma za
msingi na kuhoji endapo Serikali ipo tayari kutangaza ukomo wa watoto katika
familia.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango, Dkt. Kijaji, amesema kuwa Serikali haiwezi kuweka ukomo wa
idadi ya watoto katika familia kwa sababu linahusisha masuala ya mila, desturi
na tamaduni za Taifa.
Post a Comment
karibu kwa maoni