0
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inautaarifu umma kuwa   Tanzania inaungana na Nchi nyingine za Afrika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, tarehe 16 Juni 2017.
Chimbuko la Maadhimisho haya ni Azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1990 kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa kitongoji cha Soweto nchini  Afrika ya Kusini waliouawa tarehe 16 Juni, 1976 kutokana na ubaguzi wa rangi.
Watoto hao walikuwa wakidai haki zao za kutobaguliwa pamoja na haki nyingine za          kibinadamu ikiwemo haki ya kupata elimu bora na hivyo kupinga mifumo ya elimu ya         kibaguzi. Kufuatia tukio hili, OAU iliazimia kuwa tarehe 16 Juni ya kila mwaka iwe Siku ya Mtoto wa Afrika.
 Kupitia Maadhimisho haya, Serikali na wadau wengine tunakumbushwa kuandaa             mipango thabiti ya kuwaendeleza watoto na kukuza ufahamu wa wazazi, walezi na jamii     kuhusu  utatuzi wa changamoto zinazowakabili watoto wa Afrika na kuzitafutia ufumbuzi.  
Aidha, maadhimisho haya ni fursa ya kutathmini utekelezaji wa Sera za Taifa zinazohusu   maendeleo ya watoto kwa kuwapatia huduma stahiki ikiwa ni pamoja na afya, elimu, ulinzi na    malezi bora ili kuwarithisha stadi mbali mbali na tunu za kitaifa kwa manufaa yao, familia na taifa kwa ujumla.
Kwa mwaka huu Maadhimisho haya yatafanyika kimkoa hivyo kila Mkoa utaadhimisha       siku hii kwa kuzingatia mazingira ya mkoa husika.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa Watoto” Kaulimbiu hii inawataka wazazi, walezi, Serikali na wadau wengine kuzingatia wajibu wetu katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na maendeleo ya Mtoto  ilii awezekudhibiti changamoto ya ongezeko la vitendo vya ukatili nchini pamoja na kutoa       haki sawa kwa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote.
Wizara inatoa wito kwa  wanahabari, Asasi za Kiraia na wadau wengine  kushirikiana na Serikali katika kuadhimisha Siku hii na kuelimisha jamii kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu. Utekelezaji wa Kaulimbiu hii utasaidia  kuimarisha ulinzi, usalama wa Mtoto na kutoa haki sawa kwa watoto wote kwa lengo la kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030.
Mwisho, tunapenda kuwakumbusha Watanzania wote kutambua kuwa kila mmoja wetu   ana wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wanapata Haki zao za Msingi kuanzia katika ngazi ya   familia ambayo ni kitovu cha maendeleo ya Mtoto, jamii na taifa kwa ujumla.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top