0
Madini aina ya kinywe yaliyogundulika Tanzania ambayo hutumika kutengeneza betri, breki, kinga za mashine hivi karibuni yataanza kutumika ulimwenguni baada ya sampuli yake tani 500 kupelekwa Canada kwa ajili ya kufanyiwa majaribio.
Wakati dunia ikiendelea kushuhudia Tanzanite isiyopatikana kwingine kokote isipokuwa Mirerani, Novemba mosi, 2016 nchi ilitangaziwa kugunduliwa kwa madini mapya duniani yaitwayo ‘merelaniite’ yaliyogundulika kwenye eneo hilo lililopo mkoani Manyara.
Hayo yalibainishwa na Nkute wakati akizungumza kwa niaba ya Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko wakati wa usafirishaji uliofanywa na kampuni ya uchimbaji madini ya Mahenge Resources katika stesheni ya Tazara ya Ifakara.
Taarifa za ugunduzi wa kinywe ilibainishwa mwishoni mwa wiki na Ofisa Madini Mkoa wa Morogoro, Theresia Ntuke wakati wa uzinduzi wa usafirishaji wa madini hayo yanayopatikana Mahenge wilayani Ifakara mkoani Morogoro.
Sampuli za madini hayo zilisafirishwa kwa kutumia treni ya Tazara kutoka Ifakara kwenda Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya taratibu za kuzipeleka Canada.
Akizungumza na wananchi walioshuhudia usafirishaji wa madini hayo, Ntuke alisema kampuni hiyo ipo katika hatua ya upembuzi yakinifu wa utafiti wao ambao kiasi cha madini ya kinywe yaliyogunduliwa hadi sasa ni tani milioni 69.9.
“Tupo hapa kushuhudia uzinduzi wa usafirishaji wa sampuli ya madini ya kinywe tani 500 inayopelekwa Canada kwa ajili ya kufanyiwa majaribio ili kampuni ya Mahenge iweze kufahamu ni aina gani ya mitambo inayofaa kwa ajili ya kuanzisha mgodi wa kuchakata aina hii ya madini yaliyovumbuliwa Mahenge,” alisema.
Alisema kampuni hiyo ipo katika hatua za mwisho za utafiti na inatarajia kuanzisha mgodi mkubwa wa kuchakata madini hayo.
“Mgodi huu unategemewa kuwa na faida kubwa katika uchumi wa taifa na unaunga mkono azma ya Rais John Magufuli ya kuipeleka Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati,” alisema zaidi Ntuke.
“Kampuni hii inategemea kuzalisha tani 80,000 kwa mwaka kwa kuanzia, na uzalishaji utafikia mpaka tani 250,000 kwa mwaka.”
Ofisa Madini Mkoa wa Morogoro Ntuke alisema uzalishaji huo unakadiriwa kuchangia dola za Kimarekani milioni 100 (Sh. bilioni 226) kama kodi kwa mwaka kwa Mamlaka ya Mapato (TRA).
“Mgodi huu utatoa ajira za moja kwa moja za zaidi ya watumishi 150 pamoja na ajira zingine zisizo rasmi zinazoendana na shughuli za uchimbaji,” alibainisha.
Mwenyekiti wa Mahenge Resources, John de Vries ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Black Rock Mining kutoka Australia alisema anaamini hivi karibuni vifaa vinavyotumia kinywe vitaanza kutumia madini hayo kutoka Tanzania.
“Kuipeleka kinywe katika soko la ulimwengu ndiyo hasa sababu ya uwepo wetu hapa, kwa kawaida huwa tunaunganisha mapinduzi ya nguvu na uendelevu wa mazingira ya biashara,” alisema.
Balozi wa Australia nchini, Alison Chartres alisema wakitazama kiwango cha mitaji ambayo kampuni za nchi hiyo zimewekeza nchini wanaweza kuzungumzia kiasi cha mabilioni mengi ya dola za Kimarekani.
Alisema Australia inatambua umuhimu wa sekta ya madini ambayo inashiriki kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi na ustawi wa wananchi hivyo wataendelea kumuunga mkono Rais Magufuli.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top