Kiwango cha biashara kati ya Tanzania
na China kimefikia Dola bilioni 4.7 katika kipindi cha mwaka 2015 na kwamba
kiwango hicho kinatarajiwa kuongezeka zaidi.
Mwakilishi Mkuu Mkazi wa Masuala ya
Uchumi na Biashara, kutoka Ubalozi wa China hapa nchini, Bw. LIN Zhiyong, amesema hayo Jijini Dar es Salaam,
wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya forodha kuhusu Maboresho na Vihatarishi hatari
vya kiforodha, yanayotolewa kwa maafisa wa forodha wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania na wataalamu kutoka Chuo cha Forodha cha Shanghai-China.
Bw. Zhiyong amesema kuwa
uhusiano wa Tanzania na China ni wa kihistoria na kwamba hivi karibuni nchi
yake iliipatia Tanzania seti 3 za makontena ya vifaa vya kisasa kwa ajili ya
kufanya ukaguzi wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, vyenye uwezo mkubwa
wa kugundua pembe za ndovu, dawa za kulevya na silaha zinazosafirishwa
kimagendo kutoka ndani na nje ya nchi.
Alisema pia kuwa hivi sasa nchi yake
ni kama imeondoa kabisa kodi kwa bidhaa za Tanzania zinazosafirishwa kwenda
China hadi kufikia asilimia 97, na kwamba anatarajia kuona wafanyabishara wa
Tanzania wakichangamkia fursa hiyo na kuongeza kiwango cha bidhaa za Tanzania
zenye ubora zinazosafirishwa kwenda nchini mwake.
Bw. Zhiyong, amezishauri
Idara za Forodha za Tanzania na China kuimarisha ushirikiano na kukuza biashara
na uwekezaji kwa faida ya pande zote mbili.
Akizungumzia kuhusu sekta ya elimu,
Mtaalamu huyo wa masuala ya Uchumi na Biashara amesema kuwa hadi mwishoni mwa
mwaka uliopita, Watanzania 5,000 wako nchini China wakipatiwa mafunzo
mbalimbali kupitia Wizara ya Biashara ya nchi hiyo kwenye vyuo mbalimbali.
Alisema kuwa wanafunzi wa Kitanzania
wanaosoma nchini China
Akifungua mafunzo hayo ya majuma
mawili, Naibu Kamishna wa Maboresho ya vihatarishi hatari, kutoka Idara ya
Forodha ya Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw. James Mbunda, amesema kuwa
mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wafanyakazi wa idara hiyo wa
kukabiliana na vihatarishi vyote vya masuala ya forodha kwa bidhaa zinazoingia
na kutoka nchini kwenda nje ya nchi.
Amesema kuwa mafunzo hayo yameratibiwa
na Serikali kupitia Wizara ya Utumishi ikiwa ni hatua ya Serikali ya kuboresha
utendaji kazi wa idara hiyo kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.
Ameyataja baadhi ya masuala
watakayopewa utaalamu na wakufunzi watano kutoka Chuo hicho cha Forodha cha
Shangai wakiongozwa na Profesa wa masuala ya forodha Bi. Sun Hao, ni pamoja na
kupitia sheria mbalimbali za forodha, misamaha ya kodi, udhibiti wa biashara,
namna ya kukabiliana na watu wasio tii sheria na vigezo vya utoaji leseni.
Post a Comment
karibu kwa maoni