Mpango wa CCM wa
kutaka kusaidia wanafunzi yatima, walemavu na wenye wazazi wasiojiweza ambao
walikosa mikopo kwa ajili ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu, umeibua
maswali.
Maswali hayo yameibuka
baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kuandika katika
ukurasa wake wa Twitter kuwa wanafunzi wenye matatizo hayo wafike ofisi ndogo
ya makao makuu ya CCM iliyopo Mtaa wa Lumumba jijini hapa.
Kwa mujibu wa takwimu
za Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB), watu saba kati ya kumi walioomba
mikopo kwa mwaka 2016/17, hawakupata, hali ambayo imefanya wadau mbalimbali
kutaka hatua zichukuliwe kusaidia wengi zaidi.
Kilio hicho kimeifanya
CCM itangaze mpango huo wa kusaidia waliokosa mikopo, ikiweka vigezo vya
ulemavu, wenye wazazi wasiojiweza na yatima.
Hata hivyo, mbunge wa
Kibamba (Chadema), John Mnyika amesema hiyo ni tabia ya CCM kujijenga kichama
kupitia mapengo ambayo kimsingi yametengenezwa na Serikali yake.
Alisema suala la
mikopo ni wajibu wa Serikali, hivyo kuwapo kwa wanafunzi walioikosa, tena wenye
mahitaji maalumu kama hao, kunaonyesha haikutimiza wajibu wake.
“Utaratibu huu
unaidhalilisha Serikali kwa kuonyesha kuwa ni dhaifu na mambo muhimu kama ya
kutoa elimu yanayotakiwa kufanywa nayo, yanafaanywa na chama,” alisema Mnyika.
“Ipo haja ya kuhoji
kodi za wananchi zinafanya nini kama wao wameshindwa kuzitumia ipasavyo na
kukiachia chama kufanya hivyo,” alisema Mnyika.
Mbunge huyo alisema
ipo haja kwa Waziri wa Elimu kuliona hilo kama kashfa upande wake kwa sababu
ameshindwa kusimamia kazi zake na kumuachia mtu mwingine kufanya hivyo.
Hoja kama hiyo alikuwa
nayo Benjamini Nkonya, ambaye ni mkurugenzi mkuu wa shirikisho la watoaji elimu
wasiotegemea bajeti ya Serikali Kusini mwa Jangwa la Sahara (Ciepssa).
“Kinachofanyika ni
sawa na kupulizia manukato uvundo badala ya kuangalia namna ya kuuondoa,”
alisema Nkonya.
Alisema kwa miaka
mingi wamekuwa wakipigia kelele wanafunzi kupewa mikopo bila kujadili shule
walizosoma kwa sababu kuna ambao wanasomeshwa kwa ufadhili na unapofika wakati
wa kupata mikopo ya elimu ya juu huachwa kwa kisingizio cha kuwa na uwezo.
Nkonya alisema mwaka
2013 kwenye mkutano mkuu wa Shirikisho la Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi
(Tamongsco) uliofanyika Mbeya, walimueleza mgeni rasmi ambaye alikuwa Rais wa
Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuwa madhara ya upimaji huo wa
wanafunzi wanaostahili kupata mikopo.
Mkurugenzi huyo
alisema wakati huo shirikisho lao lilikuwa na shule na vyuo 3,400 binafsi nchi
nzima na kwa hesabu ya haraka kila taasisi ilikuwa na yatima sita inaowasomesha
bure, lakini hawakuweza kupata mikopo kwa hoja kuwa walisoma shule za kulipia.
“Asipake manukato
uvundo, suala hili liingizwe kwenye mijadala ya Serikali ili lijadiliwe ikiwa
ni pamoja na kushirikisha Tamongsco ambao alisema wapo tayari.
“Bodi ya mikopo katika
vigezo ilivyotaja mwaka wa masomo 2016/17 ni pamoja na kuwapa nafasi yatima na
wasiojiweza. Kama wapo ambao hawakupata wanaojiorodhesha leo kwa ajili ya
kupewa na CCM, bila shaka kuna mahali hapakuwa sawa, ” alisema Nkonya.
Aliishauri Serikali
ifanye kama Kenya ilivyofanya kwa kusajili yatima wote na kuwafuatilia popote
walipo ili kuepuka mkanganyiko.
Stanslaus Kadugazile,
mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania
(Tahliso), alipongeza hatua hiyo ya CCM, akisema kama hawajabagua wanafunzi
wanaotaka kuwasaidia kwa itikadi za chama wamefanya jambo la busara.
Pia, msomi mmoja
ambaye hakuwa tayari jina lake kuandikwa gazetini kwa kile alichodai ni mjadala
dhaifu, alisema jambo hilo lina maswali mengi kuliko majibu.
Alisema mpango wa CCM
haujaeleza kama ni wa nchi nzima au Dar es Salaam pekee, kwa sababu
unapozungumzia walemavu moja kwa moja umezungumzia uwakilishi badala ya kila
mmoja kufika wenyewe.
“Unaratibiwa na nani,
fedha zimetoka katika mpango upi wa chama? Anapimaje yatima na kujiridhisha
kuwa wanahitaji msaada huo? Kwa sababu wapo yatima matajiri waliorithi mali kwa
wazazi wao,” alisema msomi huyo.
Alisema kutoa elimu si
jambo la dharura, bali linahitaji mipango tena endelevu kama ilivyo kwa ulinzi
wa nchi na suala la hali ya chakula. Kwa misingi hiyo, alisema mpango huo
unahitaji kuangaliwa upya.
Wakati huohuo, Idara
ya Itikadi na Uenezi ya CCM imesema wameshapokea wanafunzi 20.
Mbali na mikopo kwa
wanafunzi, CCM imekuwa ikihamasisha wanachama wake kujikusanya katika vikundi
vya watu wanne ili kiwawezesha kupata mikopo inayotolewa na halmashauri kwa
vijana na wanawake.
Uchunguzi wa gazeti la Mwananchi ulibaini kuwa katika baadhi ya halmashauri, vijana hutakiwa kukata kadi ya CCM kwanza, jambo ambalo limefanya mikopo hiyo ipewe jina la “mikopo ya CCM”.
Post a Comment
karibu kwa maoni