Mkuu wa jeshi la polisi nchini Tanzania IGP Simon
Sirro amefunguka na kusema kuwa jeshi la polisi nchini litaendelea kuwakamata
na kuwachukulia hatua mbalimbali baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini
wenye lengo la kufanya uchochezi.
IGP Sirro ametoa kauli hiyo siku mbili baada ya
jeshi la polisi nchini kumkamata Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) Tundu
Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kwa
kutuhumiwa kutoa maneno ya kichochezi.
Aidha Sirro amedai kuwa jeshi hilo litaendelea
kuwachukulia hatua kali za kisheria ambazo ni pamoja na kuwafikisha Mahakamani
viongozi wa vyama vya siasa wanaojaribu kujitafutia umaarufu kwa kutoa kauli
zenye utata hasa zile zinazolenga kuchochea vurugu jambo linaloweza kusababisha
hali ya uvunjifu wa amani ambayo imedumu hapa nchini kwa muda mrefu.
Viongozi wa CHADEMA ndiyo wamekuwa wahanga namba
moja kukamatwa na jeshi la polisi nchini kwa tuhuma za kutoa lugha za kuudhi,
na uchochezi ambapo kwa mwezi huu wa saba pekee zaidi ya viongozi 10
wamekamatwa na jeshi la polisi kwa makosa mbalimbali.
Post a Comment
karibu kwa maoni