OMBI la Dodoma kuwa Jiji litawasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais John Magufuli ambaye ndiye mwenye Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Akizungumza na wafanyakazi wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Mkuu (CDA), kabla ya kuwapangia vituo vya kazi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tamisemi, George Simbachawene alisema ataliwasilisha ombi hilo kwa Rais ambaye ndiye mwenye dhamana ya wizara hiyo.
Awali akiwasilisha ombi hilo kwa Waziri wa Nchi (Tamisemi), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi alisema vigezo vyote wamevitimiza hivyo wanaomba halmashauri ya Manispaa ya Dodoma liwe Jiji. Kunambi alisema halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imepitia taratibu zote kwa kupitisha mapendekezo katika Kamati za Ushauri za Wilaya DCC).
“Pia tayari Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) imepitisha na taratibu imekamilisha, kwa sasa mapendekezo hayo yamewasilishwa Tamisemi,” alisema na kuongeza: “Tunaomba Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma iweze kupandishwa hadhi na kuwa Jiji kwa kuzingatia sasa Makao Makuu yamekwishahamia hapa.” Akijibu ombi hilo, Simbachawene alisema kama taratibu zote zimekamilika na vigezo vipo vya kuifanya manispaa hiyo kuwa jiji, atazifuatilia nyaraka hizo na kuzipitia na baadaye kuzifikisha kwa Rais mwenye dhamana ya wizara.
Aliwaomba watendaji wa ofisi yake kama wamepashapata nyaraka za Dodoma kuwa jiji kuzifikisha mezani kwake haraka ili kuzipitia na kuziwakilisha kwa mwenye dhamana ya Tamisemi ambaye ni Rais. Tangu mwaka jana, Serikali imahamishia watendaji wake katika mji wa Dodoma ambao hadi sasa ni Halmashauri ya Manispaa, hivyo DCC na RCC imeomba upandishwe hadhi na kuwa jiji kulingana na dhamana yake kubwa ya serikali kuhamia hapo. Rais Magufuli akiridhia Dodoma kuwa jiji litakuwa la sita nchini baada ya lile la Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Tanga na Arusha..
Post a Comment
karibu kwa maoni