0


Rais John Magufuli 
RAIS John Magufuli ameagiza watu waliojenga kwenye hifadhi ya barabara na reli, nyumba zao zibomolewe kwani sheria lazima isimamiwe, na kuagiza zianze za wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wanagoma zisibomolewe.
Aidha, amebainisha kuwa ni mateso kuwa waziri chini ya utawala wake kwa sababu inawabidi mawaziri hao saa nyingine kushiriki mateso ambayo yeye anayapata hasa linapokuja suala la kuhakikisha wananchi wanapata maisha bora. “Nasikia kuna baadhi ya watu, tena wanaCCM wanawaambia eti msibomoe, mimi naagiza bomoeni zote na tena anzeni na nyumba za wanaCCM,” alisema Rais Magufuli wakati akizindua barabara ya Kaliua – Kazilambwa iliyogharimu zaidi ya Sh bilioni 61 umefanyika siku ya kwanza ya ziara ya Rais Magufuli mkoani Tabora baada ya kukamilisha ziara yake mkoani Kigoma mapema jana.
Aidha, amempa mwezi mmoja Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kuhakikisha kuwa barabara inayounganisha Kaliua na Urambo yenye urefu wa kilometa 28 inajengwa kwa kiwango cha lami. Mbali na barabara hiyo ya Kaliua – Urambo, Rais Magufuli pia alimwagiza Profesa Mbarawa kuhakikisha ndani ya siku 45 anampata mkandarasi wa kujenga barabara ya Nyahua – Chaya yenye urefu wa kilometa 85 kwa kuwa fedha za barabara hiyo zipo tayari.
Rais Magufuli alisema wananchi wa Tabora wameteseka kwa muda mrefu kwa kukosa barabara bora, hivyo chini ya serikali yake ni lazima barabara hizo zijengwe kwa kiwango cha lami na kwa ubora unaotakiwa. “Kuongoza nchi inabidi kuwa mkorofi kidogo, ndiyo maana natoa maagizo haya hadharani, siwanyanyasi,” alisema Rais Magufuli na kuongeza: “Ninawaamini ndiyo maana natoa maagizo hayo, nisingewaamini nisingeagiza, mnafanya kazi nzuri.”
Aidha, alikemea tabia ya baadhi ya wananchi wa Tabora kuharibu misitu na kusababisha ukame, akisema watu wanakata miti ovyo kwa kuchoma mkaa na wengine kulisha mifugo hali inayosababisha maji kukauka na nyuki kukimbia. Alisema Tabora na kwa namna ya pekee Kaliua kulikuwa na hifadhi nzuri ya mazingira, lakini uharibifu wa mazingira umesababisha uzalishaji wa asali bora duniani kutoka Tabora kupungua.
“Mnafyeka mapori na kukata miti ambayo mingine iliishi zaidi ya miaka 150, halafu anayekata huo mti ana umri wa miaka 20, lakini wafugaji pia mnatakiwa kufuga kisasa kwa kupunguza idadi ya mifugo, msifuge bila mipango, nampongeza Mkuu wa Wilaya ya hapa kwa kupiga marufuku uharibifu wa hifadhi,” alisema Rais Magufuli. Akijibu hoja zilizotolewa na wananchi kuhusu zao la tumbuku mkoani humo, Dk Magufuli alisema kulikuwa na makosa yaliyofanywa na serikali na makosa yaliyofanywa na wananchi wenyewe.
Akifafanua hoja hiyo, Rais Magufuli alisema serikali ilifanya makosa kwa kuruhusu kuwepo kwa tozo nyingi kwenye mazao. Alisema tozo hizo zilisababisha kushuka bei kwa mazao hayo na kuwasumbua wananchi. Alisema kulikuwa na tozo zaidi ya 30 kwenye zao la kahawa, lakini serikali yake imejitahidi kuziondoa tozo 80 kwenye sekta ya kilimo.
“Lakini pia wananchi waliokopeshwa pembejeo kama mbolea na dawa kutoka kwenye vyama vya ushirika, hawakurudi kuuza mazao yao kwenye ushirika walikokopa fedha, walikwenda kuuza kwingine; lakini hata viongozi wa ushirika mliowachagua wengi walikuwa mchwa, walafi na majizi, hatukujenga ushirika imara,” alieleza Rais Magufuli katika hotuba zake zilizorushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Aliongeza kuwa alimwagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatilia matatizo ya tumbaku mkoani Tabora na atakapokamilisha kazi hiyo, ufumbuzi utapatikana, hivyo akawataka wananchi wawe wavumilivu. Aidha, aliwataka wananchi wa Kaliua kumpa ushirikiano mbunge wao, Magdalena Sakaya wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa kuwa anasimamia maendeleo ya wananchi.
Alisema maendeleo hayana chama na ni mara kumi uwe na mbunge wa CUF au chama kingine anayetekeleza mambo ya CCM kuliko kuwa na mbunge wa CCM anayetekeleza mambo ya vyama vingine. Akiwa mjini Urambo jana jioni, Dk Magufuli aliweka wazi kuwa ni mateso kuwa waziri chini ya utawala wake kwa sababu inawabidi mawaziri hao saa nyingine kushiriki mateso ambayo yeye anayapata hasa linapokuja suala la kuhakikisha wananchi wanapata maisha bora.
Akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara alipokwenda kufungua barabara ya Urambo – Tabora yenye urefu wa kilometa 64 iliyojengwa kwa fedha za ndani Sh bilioni 118, Dk Magufuli alisema mawaziri wake ni lazima watambue hilo, lakini pia anashukuru kwamba wote wanafanya kazi nzuri. Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi tano barani Afrika zinazojenga barabara zake kwa kutumia fedha zao wenyewe. Aidha, amewasisitiza wananchi kulipa kodi kwani ndiyo inayotumika kuleta maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, elimu bure, maji na afya. Amewataka wananchi wamuunge mkono hasa anapopambana na ufisadi kwani hakuna mtu anayejua siri za nchi kama Rais

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top