0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 25 Julai, 2017 amekamilisha ziara yake ya kikazi ya siku 7 katika Mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora na Singida kwa kufungua barabara ya Itigi – Manyoni Mkoani Singida.

Barabara hiyo inayounganisha Mikoa ya Singida, Tabora na Kigoma ina urefu wa kilometa 89.3 na imejengwa gharama ya Shilingi Bilioni 114.692, fedha ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania.

Akizungumza na wananchi wa Itigi katika sherehe za ufunguzi wa barabara hiyo Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, amesema Watanzania wana kila sababu ya kutembea kifua mbele kwa kuwa barabara hiyo pamoja na nyingine saba alizozifungua katika ziara hii zenye urefu wa jumla ya kilometa 707 zimejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 806, fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.

Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini na kwamba Serikali imeamua kuanzisha Wakala wa Barabara Vijijini kwa lengo la kuhakikisha barabara za vijijini zinajengwa kwa kiwango cha lami.

Kwa barabara ya Mkiwa – Itigi yenye urefu wa kilometa 57 na ambayo tayari zabuni ya ujenzi ilishatolewa kwa mkandarasi ili aijenge kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Shilingi Bilioni 104, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuupitia upya mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo kwa kuwa kiwango cha fedha kilichopangwa ni kikubwa ikilinganishwa na gharama halisi.

Pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa kujadiliana na Mkandarasi anayejenga barabara hiyo ili aweze kuendelea kujenga barabara kutoka Itigi kuelekea Chunya hadi Makongorosi Mkoani Mbeya.

Pamoja na wananchi wa Itigi Mkoani Singida, Mhe. Dkt. Magufuli aliyetokea Tabora amezungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake katika vijiji vya Kigwa, Kizengi na Tura Wilayani Uyui na amewataka kuendelea kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa pamoja na kuzingatia uzalishaji mazao yanayostahimili ukame kama vile uwele, mtama, viazi na muhogo ili kuepuka tatizo la upungufu wa chakula.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi wote nchini kuhamasisha wananchi kufanya kazi hususani shughuli za kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa Taifa, na ameonya kuwa kiongozi ambaye hatatekelezi agizo hilo atakuwa hafai na ataondolewa.

“Nawaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya hamasisheni watu kufanya kazi na kama kuna viongozi na watendaji wasiotekeleza wajibu huo katika maeneo yenu waondoeni mara moja” ameagiza Mhe. Rais Magufuli.

Viongozi wengine waliongozana na Mhe. Rais Magufuli katika ziara ya leo ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamis Kigwangalla, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King na Wabunge wa Mkoa wa Singida.

Mhe. Rais Magufuli amewasili katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma

25 Julai, 2017

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top