0



WIMBI la madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) limehamia mkoa wa Kilimanjaro baada ya upepo wa aina hiyo kuvuma kwa wiki kadhaa mkoani Arusha.

Hatua hiyo ya madiwani wa mkoani Kilimanjaro hasa katika ngome ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, kutikiswa inafanya madiwani waliotimkia CCM kufikia 12 baada ya jana watatu wa wilaya ya Hai.

Madiwani hao, akiwamo Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Hai, Goodluck Kimaro, walitangaza kuhama wakati wa ziara ya Katibu wa NEC ya CCM wa Itikadi na Uenezi, Hamphrey Polepole, mkoani Kilimanjaro.

Mbali na Kimaro, wengine waliojiunga na CCM ni Diwani wa Weruweru ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Weruweru, Abdallah Kassim, na Evarsit Peter wa Kata ya Mnadani.

Kama ilivyokuwa kwa wenzao wa mkoa wa Arusha, madiwani hao walidai kuwa wanajing’atua Chadema na kuhamia CCM kwa kile walichodai kuridhishwa na utendaji wa serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Magufuli.

Akizungumza katika ofisi ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro, wakati akiwapokea madiwani hao, Polepole alisema baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wamejionea kwa macho utendaji kazi wa Serikali ya awamu ya tano chini ya CCM.

Alisema kutokana na utendaji kazi huo mpaka sasa wana orodha ya baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wakiwamo wabunge, madiwani, wenyeviti wa vyama hivyo mkoa na wilaya, ambao wameomba kujiunga na CCM na muda wowote watapokewa.
“Wapinzani wamekuwa wakifanya siasa za majitaka kuwadanganya wananchi kuwa tunawanunua viongozi wao badala ya kujitafakari kwa nini wanakimbiwa. Sasa ili kudhihirisha kuwa hatuwanunui tunawapokea na wakiendelea kuleta midomo tutaendelea kuwachukua zaidi,” alisema Polepole. 

Polepole alisema wako baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani ambao walidhani wamejimilikisha mkoa wa Kilimanjaro bila kujua kuwa wako watu ambao bado wanaipenda CCM.

Aidha, Polepole alisema kuondoka kwa madiwani hao ni salamu tu kwao kwa kuwa bado kuna orodha ndefu ya viongozi mkoa wa Kilimanjaro wanaoomba kujiunga na CCM.

Aidha, Polepole alisema wanachama na viongozi wanaohamia CCM katika kipindi hiki wamekuwa wakitishiwa na kunyanyaswa na kujuhumiwa na watu mbalimbali.

Alivitaka vyombo vya usalama kuhakikisha wananchi wanakuwa salama wakati wote kwa kuwa Katiba ya nchi haimlazimishi mwananchi kuwa chama
gani.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kimaro alisema ameamua kuondoka Chadema kutokana na viongozi wake kushindwa kuheshimu demokarsia na kuendesha chama wanavyotaka.

Kimaro alisema katika hali ya kushangaza Mbunge wa Hai, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, tangu achaguliwe na wananchi hajawahi kurudi jimboni, lakini chama kinashindwa kumwajibisha kutokana na kukiongoza anavyotaka.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top