0
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Tanzania siyo lango la kupitishia dawa za kulevya kwenda nchi za nje, hivyo ameagiza ulinzi uimarishwe katika mipaka yote.
Alisema kuna tabia ya baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu kutumia Tanzania kama njia ya kupitisha dawa za kulevya kwa ajili ya kupeleka nchi za Afrika Kusini, Malawi na Zambia. Alitoa kauli hiyo juzi alipozungumza na watumishi wa kituo cha forodha cha Kasumulu kilichopo mpaka wa Tanzania na Malawi wilayani Kyela.
Waziri Mkuu alisema ili kuhakikisha jambo hilo linadhibitiwa ni vema ukaguzi wa watu wanaopita kwenye maeneo hayo pamoja na mizigo ukaimarishwa. “Endeleeni kufanya upekuzi wa kina wa magari, watu na mizigo yote katika mipaka yetu. Tanzania siyo lango la kupitishia dawa za kulevya na Serikali haitakubaliana na jambo hilo,” alisema. Pia aliwataka viongozi hao kuhakikisha biashara zote za magendo zinazofanyika mipakani, zikiwemo za kubadilisha fedha zinadhibitiwa kwa kuwa zinaikosesha Serikali mapato.
Alisema ni vema yakawepo maduka ya kubadilishia fedha katika maeneo hayo ili kudhibiti biashara hiyo ambayo kwa sasa inafanywa kimagendo huku Serikali ikikosa kodi. “Biashara za magendo zidhibitiwe katika maeneo haya na yaanzishwe maduka ya kubadilishia fedha ili biashara hiyo ifanyike kihalali. Pia imarisheni vyanzo vya mapato,” alisema.
Pia Waziri Mkuu aliwataka Maofisa wa Uhamiaji katika mikoa hiyo ya mipakani kuhakikisha wanadhibiti uingiaji holela wa raia wa kigeni kwa lengo la kuimarisha ulinzi nchini. Waziri Mkuu alisema katika baadhi ya maeneo kwa sasa zimeanza kuonekana silaha ambazo hapo awali hazikuwepo na ndizo zinazosadikiwa kutumika katika matukio ya kihalifu.
Awali, Taniel Magwaza ambaye ni Oisa Mfawidhi wa Uhamiaji alisema watahakikisha wanafanya kazi kwa weledi katika kupambana na biashara za magendo kwenye mpaka huo. Alisema mbali na kupambana na biashara za magendo pia watadhibiti uingiaji wa wahamiaji haramu kwa kushirikiana na watumishi idara zote waliopo katika mpaka huo wa Kasumulu.
Magwaza alisema katika doria zilizofanywa mwaka 2016/17 jumla ya wahamiaji haramu 87 walikamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Alisema wahamiaji hao walitokea nchi za Malawi (30), Ethiopia (47), Burundi (6) Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) (4), ambapo baadhi walirudishwa makwao na wengine walifungwa katika gereza la mkoa wa Mbeya.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewasihi Watanzania wanaofanya kazi katika viwanda mbalimbali nchini kufanya kazi kwa bidii na kuwa waaminifu. Alisema Tanzania imedhamiria kukuza uchumi wake kupitia sekta ya viwanda, hivyo ni vema watakaopata fursa ya ajira katika viwanda hivyo kuwa waadilifu.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha gesi cha Ikama kilichoko wilayani Rungwe. Waziri Mkuu alisema wakati Serikali ikiendelea kuwakaribisha wawekezaji nchini, wananchi walioajiriwa kwenye maeneo hayo wawe waaminifu.
“Mnatakiwa muwe waaminifu, msibebe kitu chochote ndani ya kiwanda bila ya ridhaa ya wamiliki kwa kuwa mtaonesha taswira mbaya kwa wawekezaji,” alisema. Alisema uaminifu wao ndio utawezesha Watanzania wengi kupata ajira kwenye viwanda hivyo ambavyo vimejengwa katika maeneo yao.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na kampuni ya TOL Gases, Mhandisi Harold Temu alisema kiwanda kina uwezo wa kuzalisha tani 46 kwa siku. Alisema gesi inayozalishwa kiwandani hapo ni ya carbon dioxide ambayo inauzwa nchini na nchi jirani za Zambia, Malawi, Zimbabwe na Congo.
Temu alisema wateja wakubwa wa gesi hiyo ni viwanda vya kutengeneza soda, bia na pia hutumika katika kuhifadhia chakula na kwenye vifaa vya kuzimia moto. Mapema Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kusindika majani ya chai cha Katumba, ambapo alisema Serikali inaimarisha ushirika wa zao hili ili wakulima waweze kupata tija.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top