0
Rais John MagufuliRAIS John Magufuli amesema anataka wala rushwa wengi, wafungwe na ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kufanya kazi bila kumwogopa mtu ili siku moja kuwe na Tanzania isiyo na rushwa na maendeleo yafi ke kwa wananchi wa kawaida.
Amesema mkazo zaidi kwa Takukuru unapaswa kuwekwa kwenye eneo la uchunguzi na uendeshaji wa mashauri ya rushwa na ingawa kauli yake inaweza kutowafurahisha wengi, lakini anataka wala rushwa wafungwe. Rais Magufuli alisema hayo jana Ikulu, Dar es Salaam katika hafla ya kumwapisha Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo.
“Kasimamie jukumu kwa uadilifu mkubwa, hasa katika suala la uchunguzi na uendeshaji, nataka wala rushwa wengi wafungwe, hilo mimi nalitaka, najua maneno kama haya hawayataki wengi kuyasikia, nataka wala rushwa wengi wafungwe, wakifungwa hawa hapatakuwa na rushwa. “Hawa wamekuwa ni walimu wa wala rushwa na msimwogope mtu yeyote, anayehusika na rushwa ni adui wangu na wa Watanzania wote.
Tunataka manufaa yanayopotea kwenye rushwa yaende kwa wananchi wa kawaida,” alisema Dk Magufuli na kuongeza kuwa anatamani ifike mahali Tanzania iwe watu wanaishi bila rushwa. “Watu wanakosa dawa, wanakosa barabara, wanakosa vitu muhimu sababu ya rushwa, hii ni dhambi kubwa, nafikiri ni dhambi kubwa, dini yoyote, mtu yeyote mwenye kupenda watu wake hawezi kutetea suala la rushwa,” alisisitiza Rais Magufuli.
Rais alihimiza ushirikiano wa Takukuru, serikali kwa ujumla wake na wananchi kila mmoja katika eneo lake kupambana na rushwa kwa nguvu zake zote. “Tukifanikiwa kupunguza rushwa kwa angalau asilimia 80, nchi yetu itafanikiwa kutatua matatizo mengi, na ni vema mtambue kuwa hatua hizi tunazochukua zimeanza kuwavutia wafadhili wengi na wawekezaji.
Na mimi nikiwa kiongozi wenu nimeamua kupambana na rushwa kikwelikweli, na ninawaomba nyote mshirikiane kuondoa rushwa katika maeneo yenu ya kazi,” alifafanua. Aidha, Rais Magufuli aliwataka viongozi wote nchini kushirikiana katika jukumu la mapambano dhidi ya rushwa ili kuepusha madhara ya tatizo hilo katika uchumi na ustawi wa jamii.
“Ukiangalia mambo makubwa tunayopambana nayo yanasababishwa na rushwa iliyosambaa kila mahali, watumishi hewa chanzo ni rushwa, dawa za kulevya ndani yake kuna rushwa, vyeti feki ndani kuna rushwa, mikataba mibovu ndani kuna rushwa, pembejeo za ruzuku ndani kuna rushwa na huko mahakamani nako ni rushwa tu,” alisisitiza.
Aidha, pamoja na hali ya kukithiri kwa rushwa, Dk Magufuli aliipongeza Takukuru kwa kazi iliyoanza kuifanya, lakini ametaka juhudi zaidi ziongezwe ili watu wote wanaojihusisha na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.
Mara kwa mara katika hotuba zake, Rais Magufuli amekuwa akieleza dhamira ya serikali kupambana na rushwa katika kila eneo ili kuhakikisha huduma za jamii na maendeleo yanapatikana. Katika eneo la watumishi hewa pekee, Mei mwaka jana, Rais Magufuli alinukuliwa akisema kuwa serikali imebaini watumishi hewa zaidi ya 10,295 na wanalipwa Sh bilioni 11.63 kwa mwezi na kama wangeendelea kulipwa kwa miaka mitano, hasara ingekuwa Sh bilioni 696.1.
Awali, Brigedia Jenerali Mbungo alimshukuru kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo na aliahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wengine wa taasisi hiyo katika mapambano dhidi ya rushwa. Kamishna wa Maadili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji mstaafu Harold Nsekela, aliwataka viongozi wote wa umma, kuhakikisha wanajaza fomu za tamko la mali kwa wakati na pia aliwataka kutoa ushirikiano kwa sekretarieti hiyo, inapochukua hatua ya kufanya uhakiki wa taarifa zilizojazwa katika fomu hizo.
Kwa upande wake, Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki pamoja na kumshukuru Rais kwa uteuzi, alisema katika mapambano dhidi ya rushwa, hakuna jiwe linalojihusisha na rushwa litakalosalia. Kairuki alisema kuna weledi na utayari wa kufanya kazi katika mapambano hayo na kuwataka wananchi wazalendo, kutoa taarifa za wala rushwa kwa namba 113 (ujumbe mfupi au kupiga) ili hatua zichukuliwe.
Kuhusu utumishi wa umma, Waziri Kairuki alimweleza Rais kuwa wataendelea kusimamia weledi na utashi kwa kufuata taratibu, sheria na kanuni katika utumishi wa umma ili kuleta tija na maslahi kwa wafanyakazi yaboreke. Naye Mkurugenzi wa Utawala wa Takukuru, Alex Mfungo, pamoja na kumshukuru Rais Magufuli kwa uteuzi wa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, alimhakikishia kuwa wataendelea kufanya kazi kwa bidii. Pamoja na kula kiapo cha kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali Mbungo pia amekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili, Jaji mstaafu Nsekela.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top