RAIS John Magufuli amewataka viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutokuwa na kigugumizi cha kuchukua hatua pale wanapokuwa na ushahidi dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
Dk Magufuli alitoa kauli hiyo jana alipotembelea na kuzungumza na wafanyakazi wa Takukuru katika ofisi za Makao Makuu ya taasisi hiyo jijini Dar es Salaam. “Kuna mambo mengi ya ovyo yanafanyika, tumehakiki pembejeo za ruzuku na kubaini madai ya Sh bilioni 48 ni hewa, tumebaini wafanyakazi hewa zaidi ya 19,500, tumebaini kaya masikini hewa 56,000 zilizopaswa kupata fedha Tasaf, tumebaini wanafunzi hewa 5,850 waliotakiwa kupata mkopo, kuna vichwa vya treni 11 vimeletwa bila kuwepo mkataba na mengine mengi, haya yote yanafanyika kwa rushwa, nataka kuwaona mnachukua hatua stahiki,” alieleza Rais Magufuli.
Alisema ana imani na Taukuru na aliwataka wafanyakazi wake kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, uzalendo na uadilifu mkubwa na kwamba serikali itafanyia kazi changamoto zinazowakabili.
Rais Magufuli alipokea masuala mbalimbali kutoka kwa wafanyakazi wa Takukuru na amewaahidi kuwa serikali itayafanyia kazi ili kuboresha maslahi yao na mazingira ya kazi. Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, Katibu Mkuu, Dk Laurian Ndumbaro na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi na wataalamu wanaosimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji, ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa na ujenzi wa barabara mbalimbali nchini, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alitoa taarifa ya maandalizi ya awali ya kuanza kwa ujenzi wa mradi wa umeme wa Stiegler’ Gorge na kwamba zabuni ya kuanza kwa ujenzi huo itatangazwa kesho Agosti 30, 2017. Rais Magufuli alisema fedha za kuanza kwa ujenzi wa mradi huo mkubwa utakaozalisha megawati 2,100 zitakazoingizwa katika Gridi ya Taifa zipo.
Post a Comment
karibu kwa maoni