0
Video queen Agness Masogange
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepokea taarifa ya mkemia wa serikali iliyoonesha kwamba sampuli ya mkojo wa Video Queen, Agnes Gerald "Masogange" una chembechembe za dawa za kulevya.
Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri amesema leo kwamba pingamizi la upande wa utetezi kuwa fomu zilizopelekwa kwa mkemia hazikufata sheria limetupiliwa mbali na mahakama imepokea taarifa hiyo ambayo itatumika kama ushahidi.
Amesema shahidi wa kwanza ambaye ni Elia Mulima anahaki ya kuandaa ripoti, kupima sampuli na kutoa ripoti mahakamani. Pia amesema Polisi walipeleka maombi kwa mkemia wa serikali na kwamba ni wazi mshitakiwa alienda kwa mkemia na askari wawili na kumpatia kontena kwa ajili ya kuweka sampuli ya mkojo.
Mpelelezi kutoka Ofisi ya Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, WP Judith ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa alishuhudia Masogange akitoa sampuli ya mkojo kwa kuwa alisimama mlangoni.
Amedai kuwa alipewa chupa ya plastiki yenye namba ya maabara 446/2017 na kumuelekeza Masogange jinsi ya kufanya ambapo alipata sampuli ya mkojo huo. Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula, shahidi huyo alidai kuwa Februari 15, mwaka huu aliitwa na Kaimu Mkuu wa Upelelezi, Ramadhan Kingai amchukue mshitakiwa Masogange na kumpeleka kwa Mkemia wa Serikali.
Amedai baada ya kuchukua aliongozana na Askari Polisi, Sospeter kwenda kwa mkemia na kwamba saa 7 mchana walifika. "Lengo la kumpeleka kwa mkemia ni kupimwa sampuli ya mkojo kwa kuwa alituhumiwa kwa kutumia au kusafirisha dawa za kulevya," alidai Judith.
Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Reuben Simwanza alimtaka shahidi huyo kueleza alikabidhiwa na nani chupa na kwamba mkojo ulikuwa na rangi ambapo shahidi huyo alieleza kuwa ulikuwa na rangi ya njano mpauko. Hakimu Wilbard Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 31, mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top