JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
Dar es Salaam, Septemba 1, 2017: Serikali ya Japan kupitia
Shirika lake la Maendeleo (JICA), imeipatia Tanzania ruzuku ya Yen milioni 69
sawa na Shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya kufanya usanifu wa kina wa awamu ya
pili ya mradi wa upanuzi wa barabara ya New Bagamoyo, kuanzia Morocco hadi
Mwenge, Jijini Dar es Salaam.
Makubaliano ya msaada huo
yametiwa saini Septemba 1, 2017, Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) kwa niaba ya Serikali, Balozi wa
Japan nchini Tanzania Masaharu Yoshida na Mwakilishi Mkazi Mkuu wa Shirika la
Maendeleo la Japani (JICA), Satoru Matsuyama.
Tukio hilo limekwenda
sambamba na kuingia makubaliano kuhusu muda wa kukamilisha mradi huo pamoja na
kupeana taarifa ya namna mradi huo utakavyotekelezwa.
Mradi wa barabara hiyo yenye
urefu wa kilometa 4.3 utahusisha barabara yenye njia nne pamoja na kuanza kwa
awamu ya nne ya barabara itakayotumiwa na mabasi ya mwendo wa haraka (BRT phase
IV).
Akizungumza baada ya kutiwa
saini wa makubaliano hayo, Dkt. Mpango amesema kuwa barabara hiyo ikikamilika
itasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto ya msongamano wa magari kutoka
na kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Ameishukuru Japan kwa msaada
huo wa awamu ya pili ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo katika awamu ya kwanza,
Japan ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 99.5. kujenga barabara ya njia nne
katika kipande cha kilometa 12.9 kutoka makutano ya barabara ya Tegeta na
makutano ya barabara ya Mwenge.
“Si mara ya kwanza kwa Japan
kuisaidia Tanzania, wanajenga barabara za juu katika makutano ya Tazara, ujenzi
wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Dodoma hadi Babati mkoani Manyara (km
188.15), Tunduru-Mangaka – Mtambaswala (km 202) na barabara ya Iringa hadi
Dodoma (259.9)” alisisitiza Dkt. Mpango.
Alisema kuwa upanuzi wa
barabara ya Bagamoyo si tu kwamba itapunguza msongamano wa magari Jijini Dar es
Salaam lakini pia utaunganisha Jiji na Bandari ya Bagamoyo ambayo ni muhimu kwa
ajili ya usafirishaji wa watu, bidhaa na huduma kutoka Jijini, mikoa ya Pwani
na maeneo mengine ya nchi.
Balozi wa Japan, Mhe. Masaharu
Yoshida ameeleza kuwa kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa awamu ya pili ya
barabara ya Morocco hadi Mwenge kumekuja baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza
iliyohusisha ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Tegeta hadi Mwenge ili
matokeo ya mradi huo yaweze kuonekana dhahiri.
Ameahidi kuwa baada ya
kukamilika kwa usanifu wa kina wa barabara hiyo, Serikali ya Japan kupitia
JICA, itasaini mkataba wa kuanza ujenzi huo Mwezi Juni mwakani.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkuu
Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Bw. Satoru Matsuyama, amesema
Japan imeamua kufadhili mradi huo baada ya utafiti kuonesha kuwa Barabara ya
Bagamoyo ndiyo yenye msongamano mkubwa wa magari ambapo inakadiriwa kuwa magari
52,000 yanapita kila siku katika barabara hiyo.
Alielezea matumaini yake
kwamba mradi huo utakapo kamilika utasaidi kukuza shughuli za kiuchumi katika
Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa ndicho kitovu cha biashara kwa maeneo mengine ya ndani ya nchi na
kimataifa na kuwaomba wataalamu pamoja na TANROADS kuharakisha usanifu huo wa
kina.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala
wa Barabara Nchini-TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale, amesema kuwa ujenzi wa
barabara hiyo hautahusisha ubomoaji wowote wa makazi ya watu wala majengo ya
biashara.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
Post a Comment
karibu kwa maoni