0
Rais John Magufuli
RAIS John Magufuli amefuta umiliki wa mashamba mawili yenye ekari 6,100 katika Wilaya ya Kigamboni, likiwemo la Amadori lenye ukubwa wa ekari 5,400 na la Nafco lenye ukubwa wa ekari 710 linalomilikiwa na mfanyabiashara, Yusuf Manji.
Pia alivunja rasmi Wakala wa Uendelezaji wa Mji wa huo wa Kigamboni (KDA) na kuitaka mamlaka hiyo kukabidhi majukumu yote ya upangiliaji na uendelezaji kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni. Uamuzi huo ulitangazwa jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kwenye kikao cha pamoja cha viongozi mbalimbali wa serikali, dini na vyama wa Wilaya ya Kigamboni kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
“Mashamba haya mawili yameshafutwa na Rais kwa sababu hayajaendelezwa kwa muda mrefu..... tafadhali sana nisione mtu anayatumia mpaka yatakapotolewa maelekezo ya Rais. Shamba la Amadori limefutwa, tunahitaji kuwa na land bank hapa Dar es Salaam, Nafco inamilikiwa na Manji ekari zaidi ya mia saba zimefutwa,” alisema Lukuvi. Lukuvi alisema Rais amefuta umiliki wa mashamba hayo kama ambavyo inaendelea kutekelezwa katika maeneo mengine nchini.
Mwezi uliopita, Rais alifuta mashamba mengine 14 pamoja na yale yanayomilikiwa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye wilayani Mvomero mkoani Morogoro na la mfanyabiashara Jeetu Patel. Sumaye pia alifutiwa umiliki wa shamba la Mabwepande jijini Dar es Salaam. Mwaka 2015, Waziri Lukuvi alitangaza kiama kwa watu wanaomiliki mashamba makubwa bila kuyaendeleza huku wakiyatumia kukopea fedha benki, kauli ambayo amekuwa akiirudia mara kwa mara.
Lukuvi alisema ana taarifa kuwa kuna mashamba mengine Kigamboni hayaendelezwi, na kumuagiza Ofisa Ardhi wa halmashauri hiyo ya Kigamboni utaratibu wa sheria uchukue mkondo wake, ikiwamo kuwafutia umiliki wahusika. Aidha, alisema mashamba hayo yaliyofutwa na Rais yanabaki kuwa akiba ya serikali na kuwataka viongozi na wananchi wa Kigamboni kulinda maeneo hayo yasivamiwe.
Lukuvi alisema eneo la shamba la Amadori limetengwa kwa ajili ya viwanda na kwamba Wizara ya Fedha na Mipango itatoa fedha kwa ajili ya kutengeneza miundombinu katika eneo hilo. “Na Rais ameelekeza eneo hilo lipangwe kwa ajili ya viwanda na Wizara ya Fedha itoe fedha ili itengenezwe miundombinu watu waje wawekeze kwenye viwanda katika eneo hilo, wote tushirikiane katika kutafuta hao wawekezaji,” alieleza Lukuvi.
Aidha, Lukuvi aliwataka viongozi wa Kigamboni kuainisha mashamba na viwanja vikubwa ambavyo watu hawaendelezi wajulikane na waanze kutozwa kodi na pia kuwaelewesha mipango ya manispaa katika eneo husika. “Kila mtu mwenye ardhi asishangae kuona watu wa manispaa wakienda kuzungumza naye na kumueleza eneo lako hili tumeamua liwe makaburi, au liwe makaburi... msifikiri mliotunza ardhi ni kama mmetunza fedha kwenye akaunti benki,” aliongeza Lukuvi.
Alisema serikali haina lengo baya katika kunyang’anya ardhi, lakini ni kwa lengo la kupangia matumizi sahihi na kuhakikisha ardhi inaendelezwa na pia inalipiwa. Alisema serikali itaanza upya kutoa orodha ya watu wanaomiliki maeneo makubwa nchini na kwamba kuanzia mwaka huu wataanza kutozwa kodi ya ardhi. Akizungumzia KDA, Lukuvi alisema kumekuwa na migogoro ya muda mrefu juu ya mamlaka hiyo huku Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile akiiomba serikali kuingilia kati suala hilo hivyo Rais amesikiliza kilio hicho.
“Leo Rais amepokea maombi yenu na ameniomba nije kutangaza kuwa kuanzia leo hakuna KDA na ameelekeza masuala yote yaliyokuwa yakifanywa na KDA, ikiwa ni pamoja na uthamini, upangaji, utoaji vibali vya ujenzi yatafanywa na Manispaa ya Kigamboni,” alifafanua Lukuvi.
Lukuvi alisema anatoa miezi sita kwa KDA kufungasha virago vyao na kukabidhi nyaraka zote, ikiwa ni pamoja na kuwaelekeza namna ya ufanyaji kazi kwa manispaa hiyo, lakini kuanzia jana hati yoyote itakayotolewa iwe imesainiwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni. Aliwataka pia kuondoa urasimu na kuhakikisha watu wanapimiwa maeneo yao na kupewa hati ndani ya mwezi mmoja. Dk Ndugulile alimshukuru Rais kwa kusikia kilio cha wananchi wa Kigamboni na kuivunja KDA, huku akiitaka halmashauri hiyo kusimamia vyema jukumu la kuipanga na kuiendeleza Kigamboni.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top