0
Displaying IMG_8616.JPGMKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, ameiomba Serikali kuipatia Mamlaka yake vitendeakazi muhimu ili kukabiliana na vitendo vya uharamia wa bomba la mafuta katika bahari ya Hindi.

Mhandisi Kakoko ametoa maombi hayo kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, aliyetembelea bandari hiyo upande wa mafuta na kuelezwa kuhusu tukio lililotokea juzi ambapo TPA wamekamata boti moja lilikuwa likitumiwa na wahalifu kuiba mafuta kutoka kwenye bomba, baharini.

Katika tukio hilo watu wasio fahamika, wakiwa na mabomu na baadhi ya vilipuzi, walilitelekeza boti lao na kutoweka kusikojulikana kwa kupigambizi baharini baada ya walinzi wa doria kuwakurupusha kwa kurusha risasi hewani.

“Tunaomba tupatiwe vitendeakazi kwa ajili ya kikosi chetu kinachofanyakazi kubwa ya kupambana na uhalifu mbalimbali bandarini hasa magari ili kukiwezesha kikosi hicho kufanyakazi yake kwa ufanisi” alieleza Bw. Kakoko

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameahidi kuipatia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari vitendeakazi ambavyo viko ndani ya uwezo wake kama Waziri ili kuongeza udhibiti wa eneo la maji ya bahari lenye bomba la mafuta.

“Ninawapongenza sana kwa kufanikisha kuwadhibiti maharamia hao ambao wamekuwa wakitumika kuharibu miundombinu ya bomba na mafuta na kuharibu mita za kupimia mafuta, nawaahidi kuwatimizia maombi yenu ya vifaa ambavyo viko ndani ya uwezo wangu” alisema Dkt Mpango’

Alisema kuwa vitendo vinavyofanywa na wahalifu hao vinakwamisha juhudi za Serikali za kuimarisha miundombinu yake na kusabisha hasara kwa wenye mafuta na kuikosesha Serikali mapato kutokana na vitendo hivyo vya kutoboa bomba na kuiba mafuta.

Mbali na kushuhudia boti lililokamatwa pamoja na vifaa vyake ikiwemo injini na magaloni ya mafuta, Dkt, Mpango alipewa maelezo kuhusu mchakato unaoendelea wa kufunga mita mpya za kupimia mafuta (flow meters).

Mhandisi Kakoko ameeleza kuwa mchakato unaendelea vizuri na kwamba huenda ukakamilika mapema mwakani hatua itakayosaidia kuongeza mapato ya Serikali bandarini hapo.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top