Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe leo ametoa pongezi kwa Spika wa
Bunge, Job Ndungai kwa kuunda kamati nzuri ya wabunge bila ya kujali
itikadi zao na kuweza kurudisha ripoti itakayosaidia serikali.
Mbowe
ameeleza hayo wakati akitoa hotuba yake katika ghafla ya kukabidhi
ripoti ya kamati za bunge la Tanzania, ambazo zilichunguza biashara ya
madini ya Tanzanite na Almasi.
"Bunge letu likiamua kufanya
kazi kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu linayo nafasi kubwa sana ya
kuisaidia serikali, kwa kuunda Kamati hizi Mhe. Spika ameisaidia
serikali, nina imani Mhe. Spika na timu yake wanatambua bunge limejaa
watu wenye uwezo mkubwa, 'experiences' tofauti ambao wakitumika
kikamilifu wanaweza wakawa msaada mkubwa kwa taifa katika utekelezaji wa
kazi za serikali", ameandika Mbowe.
Aidha, Mbowe amesema kamati hizo
zimeweza kutambua madhaifu mengi katika mikataba huku akidai imekuwa
kawaida ya kamati teule za bunge zinapokuwa zimetumwa kufanya majukumu
yake huwa zinapeleka ripoti zilizojaa ukweli ambazo kwa bahati mbaya
pengine hazitekelezwi.
"Natambua busara ya Mhe.
Spika iliyompeleka mpaka aone ripoti hizi kwa unyeti wake zisisomwe tu
ndani ya Bunge, lakini hata watu wengine ambao ni watendaji wakuu,
vyombo vyetu vya ulinzi na usalama navyo viweze kushiriki kupokea ripoti
hizi. Kwa busara hizo hizo ili ripoti hizi ziweze kupata uzito wa
kibunge, tuzijadili ndani ya Bunge ili wabunge sasa watoke na maazimio
rasmi ambayo yatakuwa ni maelekezo ya bunge kwa serikali", amesisitiza Mbowe.
Pamoja na hayo, Mbowe ameendelea kwa kusema "kwa
sababu wengi wametajwa katika ripoti hizi haki ikatendeke kwa wote,
vyombo vyote vya umma vitakavyofanya kazi ya kusimamia jambo hili au
maazimio yatakayokuwa ya bunge au maelekezo yeyote ya kibunge au
serikali, tunaomba vikafanye kazi hii kwa haki kila mmoja apate haki
inayomstahili, asionewe mtu lakini haki isiende kupindwa katika
kuwakabili wahusika na changamoto zinazowahusu"
Mbali na hayo, Mbowe amempongeza Spika
katika kufanya uteuzi wake katika kamati hizo kwa kuwa umeweza kusaidia
kupata kitu kilichokuwa bora , kamati hizo mbili zilikuwa zimeundwa na
wabunge wa kambi zote mbili.
"Mhe. Spika alipounda Kamati
teule alichanganya wabunge kutoka vyama vyote vya siasa vyenye
uwakilishi bungeni, unaona jinsi wabunge wamefanya kazi kwa pamoja siyo
kwa misingi ya kiitikadi, wamefanya kazi kama viongozi, wamefanya kazi
kama wawakilishi wa wananchi , wamefanya kazi kama watanzania na ripoti
yao ni ya watanzania", amesisitiza Mbowe.
Kwa upande mwingine, Mbowe ameomba
ushirikiano huo usiishie kwenye kamati teule tu, bali uendelee mpaka
katika kulitumikia taifa kwa kuwa wote ni watanzania na nyumba
wanayoijenga ni moja.
Post a Comment
karibu kwa maoni