Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesitushwa na kusikitishwa
na kitendo cha Mhe. Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa
Chama cha Wanasheria Tanganyika kupigwa risasi, tukio lililotokea
Septemba 7, 2017 mjini Dodoma.
Tume inalaani vikali kitendo hicho kwani ni kitendo cha uvunjifu mkubwa wa sheria na haki za binadamu.
Tukio
hili ambalo limekuja siku chache tu baada ya tukio la ofisi za
wanasheria wa IMMMA zilizoko jijini Dar es Salaam kulipuliwa kwa bomu
siyo la kawaida, na limeleta hofu siyo kwa familia ya Mhe. Tundu Lissu
pekee, bali kwa wananchi wengi nchini.
Isitoshe, matukio haya hayaleti picha nzuri kwa nchi inayoheshimu demokrasia, haki za binadamu na utawala bora.
Hivyo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora:
1.Inalitaka
Jeshi la Polisi kuhakikisha linakamilisha haraka upelelezi wa tukio
hilo na kuwapeleka wahusika katika vyombo vya sheria.
Tume
inaamini kuwa iwapo wahusika wa tukio hili watachukuliwa hatua kali
itasaidia kukomesha vitendo vya aina hii vinavyofanywa na makundi ya
watu wanaojichukulia sheria mkononi ambayo yanaonekana kujitokeza hivi
karibuni.
2.Aidha,
inapenda kukumbusha kuheshimu haki za binadamu na misingi ya utawala
bora na kuepuka ukiukwaji wa Katiba na sheria za nchi.
3. Mwisho, inamtakia Mhe. Tundu Lissu kila la kheri katika matibabu yake ili apone haraka.
Imetolewa na:
Mhe. Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Septemba 8, 2017
Post a Comment
karibu kwa maoni