#Anaandika Benny
Mwaipaja kutoka Shinyanga
Serikali
inatarajia kuajiri wafanyakazi 400 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika
kipindi kifupi kijacho ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi
katika Mamlaka hayo, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi na makusanyo ya kodi.
Ahadi
hiyo imetolewa Mjini Shinyanga na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji, wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utendaji wa Mamlaka hayo mkoani
humo.
Dkt.
Kijaji amesema kuwa taratibu zote zimekamilika na wakati wowote nafasi za ajira
zitatangazwa na kwamba nafasi hizo zimelenga kuiwezesha TRA kuwafikia watu
wengi zaidi na kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi.
“Tunatambua
changamoto ya uchache wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA ndio maana
tumeamua kuajiri wafanyakazi hao 400 ambao ni wengi kuliko kada nyingine ili
tuweze kuimarisha utendajikazi wa Mamlaka na hivyo kuongeza makusanyo ya kodi
zinazotakiwa kwa shughuli za maendeleo nchini” alisema Dkt. Kijaji
Alisema
kuwa pamoja na uhaba wa watumishi, anaamini kuwa lengo la mwaka huu la
kukusanya shilingi trilioni 17 ambazo Mamlaka hayo imepangiwa yatafikiwa na
ikiwezekana kuzidi kwa kutumia wafanyakazi waliopo.
Dkt.
Kijaji alitoa rai kwa wafanyakazi wa TRA kuwa waadilifu na kwamba
atakayebainika kukiuka maadili yake ya kazi atachukuliwa hatua kali za
kinidhamu na kisheria.
Awali
Meneja wa Mamlaka ya Mapato mkoa wa Shinyanga Bw. Jumbe Samson, alieleza kuwa
mkoa wake umepangiwa lengo la kukusanya Shilingi bilioni 18 na kwamba wanauhakika
wa kufikia lengo hilo kutokana na mikakati mbalimbali waliyojipangia ikiwemo
kusimamia ukusanyaji kodi kikamilifu katika sekta ya madini.
Kwa
upande wake, Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA Bw. Beatus
Nchota alisema kuwa Mamlaka yake imejiwekea mipango ya kufungua ofisi zake kila
wilaya hapa nchini ili kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza wigo wa
ukusanyaji wa mapato ya Serikali ili lengo walilopewa la kukusanya shilingi
trilioni 17 liweze kufikiwa.
Post a Comment
karibu kwa maoni